Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Binti wa miaka 100

Haki miliki ya picha spl
Image caption Mwanadada kama huyu

Mwanamama mmoja nchini Canada amesherekea kutimiza miaka mia moja na moja, kwa kutoboa masikio yake kwa mara ya kwanza kabisa. Mtandao wa habari wa UPI umesema mwanamama huyo wa Windsor, Ontario, amefanya hivyo kutokana na kushinikizwa na marafiki wake.

Wiki moja iliyopita, mfanyakazi katika nyumba anayoishi alimwambia aherekee sikukuu yake ya kuzaliwa kwa kuyatoga masikio yake, limeripoti gazeti la Windsor Star. "Mwingine aliniambia nichore tatoo, nikakataa kata kata" amesema mama huyo.

Mwanamama huyo alikweda katika saluni siku ya Jumatano kwa ajili ya kutoboa masikio yake. wafanyakazi katika saluni hiyo walimtoboa na kumuwekea hereni za almasi zenye uzani wa karati 14, bila ya kumdai fedha zozote. Baada ya kutobolewa masikio yake na kuvaa hereni, mwanamama huyo ambaye ametimiza karne moja alipoulizwa na gazeti la Star anajisikiaje alijibu "Ow".

Mganga wa mvua

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Nani anaweza kuzuia mvua

Waendesha mashtaka nchini Colombia wanafanya uchunguzi juu ya kwa nini watayarishaji wa michuano ya kombe la dunia la vijana chini ya umri wa miaka 20 walimlipa mganga wa kienyeji dola elfu mbili ili auzie mvua isinyeshe wakati wa sherehe ya kufunga michuano hiyo mwaka jana.

Uchunguzi huo umekuja baada ya gharama za kuandaa michuano hiyo kufika zaidi ya dola miliono moja. Katika kupekua pekua, waligundua kuwa mganga mmoja mwenye umri wa miaka sitini na nne ambaye anadai ana uwezo wa kutumia mizimu, aliapewa kazi ya kuzuia mvua isinyeshe siku hiyo. Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimekuwa vikifanya mzaha kwa kuhoji kwa nini mganga huyo hakutumiwa kupuunguza mvua kali iliyonyesha mwaka jana na kusababisha vifo vya watu mia nne sabini na saba.

Hata hivyo kutokana na tuhuma mbalimbali za rushwa zinazosakama serikali ya nchi hiyo, wengine wanasema badala ya kumsakama mganga huyo, badala yake apewe sifa kwa sababu alitekeleza kile alichoahidi. Mvua haikunyesha katika siku ya kufunga michuano hiyo, Agosti 20. Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio mganga huyo alidai kuwa, alipewa kazi ya kuzuia mvua wakati wa sherehe ya kuapishwa kwa rais wa nchi hiyo Juan Manuel Santos.

Wacheza utupu harusini

Image caption Zawadi ya harusi

Polisi nchini Uchina wamemkamata bwana mmoja aliyekodisha wanenguaji wa kike, wanaocheza bila nguo, kwa ajili ya sherehe ya harusi ya mwanae wa kiume.

Gazeti la Global Times limeripoti kuwa bwana huyo, Zhang Cheng wa jimbo la mashariki la Jiangsu, kwanza alitaka bendi ya muziki itumbuize katika harusi ya mwanaye.

Hata hivyo alipata ushauri na kuambiwa kuwa wanenguaji wanaotoa burudani murua zaidi, limesema gazeti hilo. Baada ya kutazama unenguaji wa kinadada hao wawili, bwana Zhang aliona hiyo ni burudani nzuri kwa ajili ya mwanaye katika siku yake ya harusi.

Dakika tano tu baada ya wanenguaji wao kuanza kutoa burudani yao, mamia ya wanakijiji walifurika katika harusi hiyo ili na wao waweze kushuhudia kinadada hao waliokuwa wakicheza bila ya kuvaa chochote. Polisi walilazimika kuingilia kati msongamano wa watu. Bwana Zhang alikamatwa siku ya pili, limesema gazeti hilo, ingawa mashtaka yanayomkabili baba mkwe huyo hayakutajwa.

'Zali' la mwalimu

Image caption Mwalimu Saha hakuamini anachokiona

Mwalimu mmoja nchini India alipatwa na mshituko mkubwa baada ya kukuta dola bilioni kumi kwenye akaunti yake ya benki.

Mtandao wa Thaindian News umesema, mwalimu huyo Parijat Saha, alipotazama akaunti ayke siku ya jumapili, hakuamini alipokuta mabilioni ya dola. Mshahara wa malimu huyo ni dola mia saba kwa mwezi.

Hata hivyo haijafahamika ilikuwaje kitita hicho kikaingia kwenye akaunti ya mwalimu huyo. Mwalimu Saha aliamua kupiga simu benki na kuuliza kulikoni.

Benki hiyo mara moja ilindoa fedha hizo na kuanzisha uchunguzi wa kilichotokea. Mwalimu Saha ameviambia vyombo vya habari kuwa alikuwa akitazama kama amelipwa deni lake la takriban dola mia mbili, na kukuta dola bilioni kumi badala yake. "Yaani ilinichukua dakika kadhaa kuondokana na mshtuko ulionipata" amesema mwalimu Saha.

Uza mwana lea mke

Haki miliki ya picha AP
Image caption Usiuze mwana

Bwana mmoja nchini Saudi Arabia ameamua kumuuza mwanaye wa kiume kutokana na matatizo ya kifedha aliyonayo. Bwana huyo Saud bin Nasser Al Shahry aliweka picha ya mwanae kwenye ukurasa wa Facebook, akisema bei ya mtoto wake huyo ni dola milioni ishirini.

Mtandao wa habari wa Press TV umesema baba huyo amedai kumuuza mwanaye ndio njia pekee ya kuondokana na maisha ya kimasikini. Biashara ya kukusanya madeni isiyo rasmi ya bwana huyo ilifungwa na mahakama hivi karibuni.

Bwana Al Shahry amesema aliomba serikali imsaidie fedha, laki alikataliwa kwa sababu umri wake ni zaidi ya miaka thelathini na tano, umeripoti mtandao wa Mail online. Amesema akifanikiwa atatumia fedha hizo kumtunza mke wake na mwanaye mwingine wa kike.

Na kwa taarifa yako....

Chakula pekee kisicho oza ni asali...

------------------

Tukutane wiki ijayo..... panapo majaaliwa..

Taarifa kutoka mitandao mbalimbali ya habari duniani