Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

MTOTO NDANI YA POCHI

Image caption Pochi ni ya kuwekea hela..

Polisi nchini Marekani wanamshikilia mama mmoja baada ya kukuta ameficha mtoto mchanga ndani ya pochi yake.

Polisi katika visiwa vya Virgin wamesema walikuwa katika ukaguzi wa kawaida barabarani na kumsimamisha mwanamama huyo majira ya saa tatu na robo asubuhi siku ya Jumanne.

Mtandao wa cnews.com umesema afisa wa polisi alimsimamisha mwanamke mmoja na kutaka kuona leseni yake lakini mara akasikia sauti ya mtoto akilia.

Polisi huyo hakuweza kumuona mtoto lakini akawa akiendelea kusikia sauti ya mtoto, na hivyo kumuuliza mama huyo yuko wapi mtoto anayelia.

Polisi wamesema mama huyo alifungua zipu ya pochi yake na kumtoa mtoto mchanga wa kike.

Mwanamama huyo amesema alijifungua mtoto huyo wiki moja iliyopita akiwa nyumbani kwake.

Mtoto huyo amepelekwa hospitali na mama huyo huenda akakabiliwa na mashtaka ya uhalifu kwa kutompeleka hospitali mwanaye, baada ya kujifungua.

WAZAZI WASUSA MTOTO WA KIKE

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mji wa Jodphur kulikotokea sakata hilo

Wazazi nchini India waliosusa kumchukua mtoto wao wa kike, kwa madai kuwa mtoto wao aliozaliwa ni wa kiume, hatimaye wamerejea kumchukua, baada ya vipimo vya DNA kuonesha mtoto huyo wa kike ni wa kwao.

Wazazi hao walidai kuwa mtoto wao ni wa kiume na wamebadilishiwa na kupewa wa kike. Taarifa ya BBC imesema watoto wawili walizaliwa katika muda unaofanana katika hospitali moja mjini Jodphur wiki moja iliyopita.

Habari zinasema mchanganyiko wa watoto ulitokea na sakata la kugombea mtoto wa kuime likaanza kati ya familia mbili. Suala hilo lilipelekwa mahakamani na amri ya vipimo vya DNA kutakiwa kuchukuliwa ili kutatua utata huo.

Katika kipindi chote hicho mtoto wa kike alikuwa amesalia hospitali, huku wa kiume akiwa anagombewa na familia hizo mbili. Wazazi hao Bwana na Bibi Chain Singh, hatimaye walikubali matokeo ya vipimo na kurejea hospitali kwenda kumchukua kichanga wao wa kike.

MKATA NYWELE ABAMBWA

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Marufuku kutembea na mkasi

Bwana mmoja hapa Uingereza amepigwa marufuku kupita mitaani huku akiwa amebeba mkasi.

Polisi wamesema bwana huyo Darren Dixon wa mjini Salford, Manchester alikutwa na hatia ya kukata nywele wasichana wawili. Mtandao wa habari wa MSN umesema Bwana huyo alikuwa akinyatia wasichana mitaani na kuwakata nywele kimyakimya.

Mahakama imempa bwana huyo hukumu ya kutumikia jamii kwa miaka mitatu na pia kupigwa marufuku kubeba mkasi na vifaa vyovyote vinavyotumiwa na vinyozi mitaani. Polisi wamesema katika tukio moja msichana mmoja aligundua kuwa alikuwa akifuatwa kwa karibu na bwana Dixon, na alipoongeza mwendo na Dixon naye akamfuata, na mara alisikia mlio kwa mkasi ukikata.

Msichana huyo amesema alipogeuka, aliomuona mtu akiokota nyewele zake na kukimbia. Kachero wa polisi Konstebo Lawrence Gallagher amesema bwana Dixon hakusema kwa nini alikuwa akikata nywele za wasichana hao.

WASICHANA WAGEUKA WAVULANA

Image caption Mapacha wabadili jinsia (sio pichani)

Wasichana wawili mapacha wa kichina wamefanikiwa kuwa mapacha wa kwanza kubadili jinsia na kuwa wanaume.

Kinadada hao kutoka jimbo la kusinimagharibi mwa uchina la Yunnan walifanyia ubadilishwaji wa jinsia zao katika hospitali ya kijeshi ya mjini Shanghai. "Shughuli ya kuwabadili kutoka wanawake kuwa wanaume imekwenda vizuri" amesema Daktari Zhao Yede Daktari aliyewafanyia mabadiliko hayo.

Gazeti la Shanghai Daily limesema pacha mmoja ameruhusiwa kurejea nyumbani wakati mwingine bado anapata matibabu hospitalini.

Madaktari wamesema kinadada hao mapacha walikuwa wakipenda kuvaa nguo za kiume, na waliweka ahadi ya kutofunga ndoa hadi watakapo kuwa wanaume. Gazeti la Sun limewakariri wakisema mapacha hao wamekamilisha ndoto yao ya muda mrefu. Mmoja wa mapacha hao amesema hawakutaka habari zao zijulikane kwa sababu wanaweza kufukuzwa kazi.

KUKU KATAMIA BATA

Image caption Kasheshe kwenye maji

Kuku mmoja nchini Marekani ametotoa vitoto vya bata baada ya kutamia mayai ya bata kimakosa.

Kuku huyo aitwaye Hilda, alitamia mayai hayo akidhani ni ya kwake. Gazeti la Daily Mail limesema kuku huyo aliyatamia mayai hayo matano kwa muda wa mwezi mzima, bila kufahamu kama sio ya kuku.

Mmiliki wa kuku huyo, mfugaji Philip Palmer amesema hata kifaranga cha kwanza cha bata kilipotoka, kuku huyohakukata tamaa na aliendelea kutamia na sasa ni kama mama yao.

Mahala pekee kuku huyo anahisi kuna musheli ni wakati vifaranga vya bata vikiingia ndani ya maji na kuku huyo kushinda kuwafuata. Bwana Phillip amesema kuku huyo ameonesha kutojali na vifaranga vya bata hao humfuata kila mahali.

Mfugaji huyo amesema huenda kuku huyo bado hajafahamu kama vifaranga vyake ni bata, na hata vifaranga vyenyewe havijui kama mama yao ni kuku.

Image caption Mitindo mingine ya nywele sio mchezo

Bwana mmoja nchini Marekani ametupwa gerezani kwa miaka mitano baada ya kumpiga risasi msichana mmoja akidhani ni ndege.

Gazeti la Daily Sentinel limesema Bwana huyo Derrill Rockwell alidhani ni ndege aliyekuwa akiwasumbua sana paka wake.

Msichana huyo alikuwa amepaka rangi nyekundu nyewele zake na kufanana na ndege wenye vibwenzi vyekundu.

Bwana Rockwell amewaambia polisi kuwa baada ya kusikia paka wake wakikimbia alichukua bunduki yake na kwenda kumsaka ndege huyo, na kwa umbali wa kama futi tisini alimuona msichana huyo akipita na nywele zake nyekudu, na akadhani ni ndege.

Lakini baada ya kufyatua bunduki yake,bwana huyo amesema akaona ndege huyo hajaruka na badala yake alisikia mayowe ya msichana.

Kaimu hakimu Jason Conley amesema bwana huyo hakuwa na nia ya kumpiga risasi dada huyo, bali kweli alikuwa akitaka kutisha tu ndege.

Taarifa zinasema baada ya kusikia ukelele huo bwana Rokwell aligundua kuwa amempiga risasi binaadam na sio ndege. Gazeti limesema msichana huyo mwenye umri wa miaka ishirini na tatu alinusurika, lakini ameuhama mji wa Colorado.

Na kwa taarifa yako........... Mchwa hujinyoosha wanapoamka asubuhi.

Nawatakia Pasaka Njema !!

Tukutane wiki ijayo.... panapo majaaliwa......