Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Nzi wawili tu

Mamlaka nchini Uchina zimeanzisha sheria mpya ya vyoo vya umma.

Sheria hiyo inakataza choo kuwa na zaidi ya nzi wawili kwa wakati mmoja.Sheria hiyo iliyowekwa na halmashauri ya mannispaa ya jiji la Beijing inalenga kuhakikisha hali ya usafi katika vyoo vinavyotumiwa na jamii.

Hata hivyo haijawekwa wazi ni hatua gani zitachukuliwa iwapo nzi wa watu atakutwa chooni.

Sheria nyingine ni kuhakikisha vyoo vinasafishwa kila mara na matumizi ya vifaa vyakisasa na mafunzo ya kutosha kwa watu wanaovitazama vyoo hivyo.

Mwandishi wa BBC mjini Beijing amesema sheria hizi mpya ni mahsusi kusaidia watu wengi mjini humo ambao hawana vyoo majumbani mwao na wanategemea vyoo vya umma. Bila shaka watakuwa wakitazama huko na huko kutafuta nzi wa tatu yuko wapi..

Tembo kuwa pweza

Tembo mmoja nchini Poland anatarajiwa kuchukua nafasi ya Pweza Paul kwa kutabiri matokeo ya michuano ya maataifa ya Ulaya yanayoanza hivi karibuni.

Tembo huyo anayejulikana kama Citta mwenye umri wa miaka thelathini na mitatu atakuwa akitumia mkonga wake kubashiri timu itakayoshinda.

Habari kutoka Warsaw zinasema ubashiri wa kwanza utafanywa tarehe sita mwezi Juni, siku mbili kabla ya kuanza kwa michuano hiyo. Tembo huyo alifanya kituko wakati akitambulishwa kwa waandishi wa habari, baada ya kuumeza mpira wa miguu uliokuwepo mezani.

Mkurugenzi wa hifadhi ya wanyama ya mjini Warsaw Teresa Grega amesema tembo huyo alitabiri ushindi wa Chelsea dhidi ya bayern Munich katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya hivi karibuni. Tembo huyo atatabiri mshindi kati ya Poland watakaopambana na Ugiriki Juni nane.

Atapewa matunda matatu, mawili yakiwa na majina ya timu hizo mbili, na tunda la tatu kwa ajili ya kutabiri sare. Tembo huyo alizaliwa India, akaishi Ujerumani kabla ya kwenda Austria, halafu Uhispania na hatimaye kuhamia Poland. Bi Gregga amesema tembo huyo anapenda sana kutazama soka.

Noti taka

Bwana mmoja nchini Marekani ameingia matatani baada yakudondosha noti ya dola moja barabarani.

Bwana huyo, John davis wa Cleveland, amesema alikuwa akijaribu kutoa sadaka kwa mtu aliyekuwa barabarani.

Davis ambaye alikuwa ndani ya gari yake, alifungua dirisha na kutoa noti kadhaa za fedha ili kumpa mtu aliyekuwa akiomba msaada.

Kwa bahati mbaya, moja kati ya noti alizokuwa akizitoa ilipeperushwa na upepo. Muda si mrefu, alitoea polisi na kumkamata bwana Davis kwa kosa la kurusha taka barabarani.

"Nimekuona ukitupa karatasi" amekaririwa polisi huyo akimwambia bwana Davis. Msamaria mwema huyo amepigwa faini pamoja na gharama za mahakama zinazofika dola mia tano.

Atoroka na gari la wagonjwa

Mwanamama mmoja aliyekuwa amelazwa hospitali, alichoshwa na maisha ya hospitalini na kuamua kuiba gari la wagonjwa na kutoroka nalo.

Mwanamama huyo Heather Sullivan wa Buffalo, New York, alikataliwa kwenda nyumbani kwa kuwa hali yake haikuwa njema sana kiafya, ingawa mwenyewe alikuwa akitaka kuondoka.

Taarifa zinasema mwanamama huyo alinyata na kuiba gari la kubebea wagonjwa la hospitali ya Erie County, na kuondoka kwa kasi kubwa. Alianza kufukuzwa na polisi.

Mwanamama huyo alikuta gari la kubebea wagonjwa likiwa limeegeshwa nje ya hospitali huku fungua za gari hilo zikinin'ginia kwenye kiwashio.

Polisi wa Buffalo wamesema mwanamke huyo aliokuwa akiendesha gari hilo kwa mwendo wa kasi na wa hatari, huku akikosa kosa kugonga wapita njia. Hatimaye gari hilo lilipoteza mwelekeo na kupunduka, na mwanamama huyo kukamatwa.

Ameshtakiwa kwa kuhatarisha maisha ya watu, na kuiba gari. Hasara aliyosababisha imefika dola laki moja.

Faini kwa mluzi

Mwanamama mmoja nchini Ujerumani amepigwa faini, baada ya kupiga mluzi kwenye simu yake na kusababisha maumivu kwa mtu aliyekuwa akizungumza naye.

Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka sitini na moja, alikuwa amechoshwa kupigiwa simu na kampuni zilizokuwa zikimshawishi anunue bidhaa mbalimbali.

Mwanamama huyo wa Pirmasens, katika eneo la Rhineland amesema alikuwa amechoshwa na bughudha za wauza bidhaa waliokuwa wakimpigia simu kila mara kumshawishi anunue bidhaa zao. Siku ya siku alipopigiwa simu, aliamua kupiga mluzi kwa nguvu kwa mtu aliyempigia simu kiasi cha kumsababishia maumivu ya masikio. Mwanamama huyo amepigwa fani ya karibu dola mia tisa.

Alipofikishwa mahakamani alimwambia jaji kuwa alikuwa amechukizwa mno na simu za wafanyabiashara.

Na kwa taarifa yako.........Fani kongwe zaidi duniani ni ukunga na uganga wa kienyeji.

Tukutane wiki ijayo.... panapo majaaliwa....