Huwezi kusikiliza tena

Hali yatokota mjini Kiev, Ukraine

Upinzani nchini Ukrain umeapa kutotoka uwanja wa uhuru wanakoendeleza maandamano hayo.

Wakuu kutoka umoja wa Ulaya wameshtumu vikali rais wa Ukrain Viktor Yanukovych, kwa makabiliano makali baina ya polisi na waandamanaji yanayoingia siku ya pili sasa .

Waziri Mkuu wa Poland , Donald Tusk, amesema atapendekeza Ukrain iwekewe vikwazo vya kiuchumi huku yule wa Sweden Carl Bildt akiongeza kuwa damu ya watu 25 waliokufa katika maandamano hayo iko mikononi mwa Yanukovych.

Vile vile wameutaka upinzani kuzuia machafuko zaidi ambayo yanasambaa kwengineko nchini humo.

Kwingineko, Rais wa Ufaransa, Francois Hollande na chancela wa ujerumani, Angela Merkel ambao wamekuwa wakikutana mjini Paris wametoa taarifa ya pamoja kulaani ghasia nchini Ukraine.

Wanasema wamechukizwa na viwango vya juu vya ghasia ambazo hazikubaliki wala hazistahili kutokea nchini humo.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Muungano wa Ulaya, watakutana mjini Brussels ubelgiji kujadili swala la vikwazo dhidi ya maafisa wa serikali ya Ukraine kwa umwagikaji damu.

Serikali ya Urusi imeweka wazi kuwa inalaumu kinachofanyiwa waandamanaji na viongozi wa Ulaya wanaodaiwa kuchochea hali.

Waziri wa mambo ya nje wa Poland, Radoslaw Sikorski, atawakilisha Muungano wa Ulaya kwa mkutano wa kidiplomasia mjini Kiev.