Rais Zuma aapishwa kwa muhula wa pili

Rais Jacob Zuma Haki miliki ya picha Reuters

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ameapishwa kwa muhula wa pili wa uongozi.

Maelfu ya wafuasi, wakipepea bendera za taifa, walishangilia ndege za jeshi za Afrika Kusini zilipopita juu ya uwanja wa sherehe.

Viongozi wa nchi 20 walikuwako katika sherehe hiyo.

Katika hotuba yake ya kutawazwa Rais Zuma aliahidi kuwa serikali yake itakuza uchumi na nafasi za ajira.

Chama chake cha ANC kilishinda uchaguzi awali mwezi huu ambapo kilipata kura zaidi ya asili-mia-60.

Hii ni mara ya tano kwa chama cha ANC kushinda katika uchaguzi na kimeongoza nchi tangu utawala wa ubaguzi wa rangi kumalizika.