Regina Mziwanda wa BBC akizungumza na mtangazaji wa zamani wa BBC ambaye sasa ni mkurugenzi wa Under The Same Sun
Huwezi kusikiliza tena

Mtoto mwingine atekwa Chato

Image caption Vicky na Regina

Suala la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania limechukuwa sura mpya kaskazini Magharibi mwa nchini hiyo,huku matukio ya kuuawa na kuchukua viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi yakipungua,kumeibuka mtindo mpya wa utekaji wa watoto wenye ulemavu wa ngozi na kutokomea nao kusikojulikana .mwandishi wetu wa Dar Es-Salaam Regina mziwanda anaarifu zaidi.

Wakati Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza likiendelea kumsaka mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ,Pendo Emmanuel mwenye umri wa miaka minne kwa siku ya 51 sasa , ambaye aliibwa katika kijiji cha Ndami, Kwimba na watu wasiofahamika Desemba 27, mwaka wa jana, mtoto mwingine albino ameibwa mbele ya wazazi wake katika kijiji cha Ilelema, wilayani Chato, Geita.

Mtoto huyo, Yohana Bahati, mwenye umri wa mwaka mmoja, aliibwa usiku wa kuamkia jana, akiwa amebebwa na mama yake, Esther Bahati (30), ambaye alivamiwa na watu hao na kupigwa mapanga akiwa jikoni kisha kuporwa mtoto huyo.

Mama huyu alijitahidi kumtetea mtoto wake asichukuliwe kutoka katika mikono yake bila mafanikio na kuambulia majeraha makubwa, na kulazwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando mkoani Mwanza kaskazini mwa Tanzania ,alipokelewa hospitalini hapo kama mgonjwa wa rufaa kutoka hospitali ya Geita.Akiwa na hali mbaya baada ya kukatwakatwa kwa mapanga na watekaji hao na kusababisha kuvuja damu na mapigo ya moyo kushuka.

Serikali ya Tanzania iliunda kikosi maalumu kwa ajili ya kupambana na vitendo vya ukatili wanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi –Albino- na huku ikitangaza pia kupiga marufuku wapiga ramli wote ambao wanaelezwa kuchangia mauaji ya watu hao.