Muhtasari: Habari kuu leo Ijumaa

Miongoni mwa habari kuu leo, Hillary Clinton amekubali uteuzi na akamkebehi Donald Trump, raia watatu wa Nigeria wameuawa Indonesa baada ya kupatikana na makosa ya kulangua dawa za kulevya.

1. Clinton akubali uteuzi na kumshutumu Trump

Haki miliki ya picha Reuters

Hillary Clinton amekubali rasmi kuwa mgombezi wa Urais wa Marekani kupitia chama cha Democratic, huku akisema wakati wa kupambana na mpinzani wake sasa umeanza rasmi.

Alitoa wito kwa wanachama wote wa Democratic kuungana naye huku akimkebehi mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump, katika madai yake kuwa ni yeye pekee anayeweza kuyasuluhisha matatizo ya Marekani.

Alisema kuwa Wamarekani hufanya kazi kwa pamoja kyatatua yote yanayonufaisha taifa.

2. Ujenzi wa kinu cha nyuklia Uingereza wacheleweshwa

Mpango wa Uingereza wa kujenga kinu cha kwanza cha kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za kinyuklia baada ya zaidi ya miaka 20 umecheleweshwa na Serikali ya Uingereza, saa chache baada ya kampuni ya nishati ya Ufaransa, EDF, kukubali kuendelea na shughuli hiyo.

Waziri Mpya wa Biashara wa Uingereza, Greg Clark, alisema alitaka kuchunguza kwa makini mpango huo kabla ya kuunga mkono.

3. Raia watatu wa Nigeria wauawa Indonesia

Haki miliki ya picha Reuters

Maafisa wa Indonesia wamesema kuwa wametekeleza mauaji ya wafungwa wanne waliohukumiwa baada ya kupatikana na madawa ya kulevya.

Naibu wa Mwanasheria Mkuu alisema raia watatu wa Nigeria na mmoja wa Indonesia walipigwa risasi katika gereza la Kisiwa cha Nusa Kambangan.

4. Sauti ya aliyeshambulia padri Ufaransa yasikika

Haki miliki ya picha Reuters

Jarida moja la Ufaransa limesema kuwa limesikia sauti za Adel Kermiche, mmoja wa washambulizi wawili waliomwua padri mmoja mkongwe mnamo Jumanne.

Taarifa iliyorekodiwa kabla ya mauaji hayo ina sauti ya Kermiche anayeeleza alichokusudia kufanya.

5. Wanasayansi Singapore waunda ubongo bandia

Wanasayansi wa Singapore wanadai kuwa wametengeneza ubongo bandia wa mwanadamu kwa mara ya kwanza.

Wanasema kuwa ubongo huo mdogo utawapa nafasi bora zaidi ya kuelewa jinsi ya kuwasaidia wanaougua maradhi ya kutetemeka yajulikanayo katika Kiingereza kama Parkinson na pia kuchunguza zaidi dawa zinazotengenezwa kukabiliana na maradhi hayo.

Mada zinazohusiana