Barcelona 4-2 Leicester City: Ahmed Musa afunga mabao mawili

Ahmed Musa akisherehekea kuifungia Leicester City dhidi ya Barcelona

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Ahmed Musa alifunga mabao 13 katika mechi 30 za ligi alizochezea CSKA Moscow msimu uliopita

Mchezaji ghali zaidi kununuliwa na Leicester City Ahmed Musa, aliyenunuliwa pauni milioni 16 na kuvunja rekodi ya klabu hiyo, amewafungia mabao yote mawili katika mechi ambayo wamefungwa 4-2 na Barcelona katika michuano ya Kombe la Kimataifa la Klabu.

Munir alifungua ukurasa wa mabao kupitia pasi iliyotoka kwa Lionel Messi kabla ya nyota huyo wa Argentina muda mfupi baadaye kumuandalia pasi safi Luis Suarez aliyeongoeza la pili katika mchezo huo uliochezewa uwanja wa Friends Arena mjini Stockholm, Sweden.

Munir aliongeza la tatu, kabla ya Musa kukomboa bao moja.

Musa alifanikiwa kukomboa la pili lakini nguvu mpya wa Barca Rafa Mujica, mwenye umri wa miaka 17 pekee, akaifungua Barcelona la nne dakika za mwisho mwisho.

"Msimu uliopita Leicester walishangaza sana katika soka ya Ulaya, na hii ndiyo sababu inayomfanya kila mtu kuupenda mchezo huu," meneja wa Barcelona Luis Enrique alisema baadaye.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Lionel Messi hakufunga dhidi ya Leicester lakini alichangia ufungaji wa mabao matatu ya Barca

Mshambuliaji Jamie Vardy, aliyeongeza muda wa mkataba wake kwa miaka minne mwezi Juni, na Riyad Mahrez, ambaye amehusishwa na kuhamia Arsenal, wote walianza kwenye kikosi cha Leicester kitakachokabiliana na Manchester United katika mechi ya Ngao ya Jamii uwanjani Wembley siku ya Jumapili.

Upande wa Barca, kando na Messi na Suarez, kulikuwa na nyota wengine kama vile Javier Mascherano na Sergio Busquets.

Leicester wataanza kutetea taji lao la Ligi Kuu ya England dhidi ya Hull City ugenini mnamo tarehe 13 Agosti.