Shehzana Anwar, Mkenya pekee mfumaji mshale Rio

Shehzana Anwar

Chanzo cha picha, BBC Sport

Maelezo ya picha,

Shehzana Anwar atashuka uwanjani tarehe 6 Agosti

Mamake mzazi ndiye mkufunzi wake, na licha ya kupoteza ajira yake, mchezo wa kufuma mshale umekuwa tegemeo la Shehzana Anwar, Mkenya mwenye umri wa miaka 26.

Ndoto ya Shehzana, kushiriki Rio, ilitimia mapema mwaka huu na hivyo basi kumwezesha kuwa Mkenya pekee atakayepiga foleni kufuma mshale kwenye michezo ya Olimpiki.

"Nilianza mchezo huu kama mapendeleo, lakini baadaye kipaji changu kiligundulika nilipoanza kuibuka mshindi katika mashindano tofauti,'' Alieleza.

Shehzana maarufu 'Kuki', alifuzu kushiriki kwenye Olimpiki baada ya kupata pointi 601 ambayo ni alama iliyohitajika kufuzu. Aidha, hali hii imemfanya Shehzana, kuandikisha alama 610 iliyo sawa na rekodi ya mchezo huo nchini Kenya.

Kulingana naye, licha ya mchezo huo kutokuwa na umaarufu nchini Kenya, amekuwa akijitahidi kwa muda mrefu kuiwakilisha Kenya kwenye Olimpiki.

''Mchezo huu haufahamiki sana Kenya na hautiliwi mkazo kama michezo mingine, lakini nia yangu ni kuiweka Kenya kwenye ramani ya kimatiafa ya mchezo huo,'' anasema.

Shehzana, ambaye pia ni mtoto wa bingwa wa mbio ya magari ya langalanga nchini Kenya, Azar Anwar, atakuwa akiwania medali baada ya kuwa Mkenya wa kwanza wa kujikatia tiketi ya Olimpiki kwa njia ya kufikisha alama zilizohitajika.

Binti huyo ambaye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne, alianza kushiriki mchezo huo akiwa na umri wa miaka 13.

Kupoteza kazi

Shehzana ambaye alisomea kozi ya saikolojia, alipoteza kazi yake baada ya kuhitajika pakubwa kufanya mazoezi zaidi ili kufuzu kwa Olimpiki.

''Nilipoteza kazi yangu hapa Nairobi kwa sababu ilikuwa vigumu kuendesha kazi na maandalizi ya mchezo wa kulenga Shabaha.

Chanzo cha picha, Shehzana Anwar / Facebook

Maelezo ya picha,

Shehzana Anwar atakuwa mmoja wa watakaotegemewa na Kenya kushinda nishani

Mbali na wanariadha, waogeleaji, wawakilishi wa raga na kurusha mkuki, Shehzana atakuwa mmoja wa wanamichezo wa Kenya wanaoshiriki Olimpiki ambao wanabeba matumaini ya wakenya ya kuzoa medali Rio.

''Malengo yangu ni kuiwakilisha Kenya vyema na sina wasiwasi kuhusu wapinzani wangu, nitafanya vyema,'' anasema.