Arsenal yaichapa Man City

Theo Walcott

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Arsenal itakufungua msimu ujao dhidi ya Liverpool siku ya Jumapili

Arsenal ilitoka nyuma na kuichapa Manchester City mabao 3-2 katika mechi ya kirafiki kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu ya uingereza EPL juma lijalo.

Mechi hiyo ilikuwa ya mwisho ya kujipima nguvu kabla ya kipenga cha kuanza kwa msimu mpya wa EPL.

Sergio Aguero ndiye aliyefunga bao la kwanza katika mechi hiyo ilichezwa katika uwanja wa Gothenburg.

Hata hivyo Alex Iwobi, Theo Walcott na Chuba Akpom wakaifungia The Gunners.

Vijana wa kocha Pep Guardiola walijifurukuta na kufunga moja la kupunguza aibu kupitia kwa Kelechi Iheanacho.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Arsenal wakishabikia ushindi dhidi ya Man City

Licha ya ushindi huo kocha wa Arsenal alisalia akijikuna kichwa baada ya Gabriel kuondolewa uwanjani kwa machela akiwa amejeruhiwa.

Wakati huo huo vibonde wao katika ligi kuu ya Uingereza Chelsea hawakuwa na afueni kwani pia wao walimpoteza John Terry aliyejeruhiwa katika mechi ya kirafiki dhidi ya Werder Bremen.

The Blues waliibuka washindi kwa mabao 4-2.

Katika mechi nyingine Liverpool iliambulia kichapo cha 4-0 mikononi mwa Mainz siku moja tu baada ya kuiduwaza Barcelona kwa kichapo sawa na hicho.