Wakenya watano kuwakilisha Marekani Olimpiki Rio

Paul Chelimo

Chanzo cha picha, PAUL CHELIMO / TWITTER

Maelezo ya picha,

Mwanariadha Paul Chelimo ambaye alijiunga na jeshi la Marekani

Wanariadha watano waliozaliwa nchini Kenya ni miongoni mwa wanariadha wanaowakilisha Marekani katika michezo ya Olimpiki inayoendelea mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Wanne, Hillary Bor, Paul Chelimo, Shadrack Kipchirchir na Leonard Korir, pia ni wanajeshi katika jeshi la Marekani. Mwingine Bernard Lagat alibadili uraia mwaka 2004.

Hatua yao ya kujiunga na jeshi ilirahisisha kukubaliwa kwao kuwa raia wa taifa hilo.

Mwezi uliopita, Chelimo aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Nilipokuwa na umri wa miaka 15, mamangu aliniambia jitafutie kundi la kuwa ukikimbia nalo la sivyo utajipata mpweke karibuni. Hivi karibuni nitatimu miaka 30 nikiwa bingwa."

Chelimo hushindana katika mbio za mita 5,000.

Mwanariadha huyo alizaliwa Iten, Kenya, na alishindania Chuo Kikuu cha North Carolina mjini Greensboro kabla ya kujiunga na jeshi la Marekani.

Shadrack Kipchirchir na Leonard Korir watashiriki mbio za mita 10,000.

Korir ni mzaliwa wa Iten na alikuwa katika Chuo cha Iona kabla ya kujiunga na jeeshi.

Kipchirchir anatoka Eldoret, Kenya na alikuwa katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Oklahoma kabla ya kujiunga na jeshi 2014.

Chanzo cha picha, PAUL CHELIMO /TWITTER

Maelezo ya picha,

Bernard Lagat na Paul Chelimo

Bor, atakayeshindana katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzo na maji alitoka Eldoret na alishindana katika chuo kiku cha Jimbo la Iowa kabla ya kujiunga na jeshi 2013. Ndugu zake wawili pia wamo kwenye jeshi la Marekani. Bor huhudumu katika kambi ya jeshi la Fort Carson, Colorado.

Bernard Lagat alizaliwa Kapsabet, Kenya na aliwakilisha Kenya mashindano ya kimataifa hadi alipobadilisha uraia mwaka 2004.

Alishinda shaba Olimpiki za Sydney 2000 na fedha Olimpiki za 2004 mbio za mita 1,500.

Kwa sasa ana umri wa miaka 41 na alimshinda Chelimo mbio za kufuzu kwa Olimpiki tarehe 8 Julai katika uwanja wa Hayward Field mjini Eugene, Oregon.