Timu ya Kenya ya raga yashindwa tena Olimpiki Rio

Shujaa

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Kenya imeshindwa mechi zote nne ilizocheza Rio

Timu ya Kenya ya raga ya wachezaji saba kila upande imeendelea kuandikisha matokeo mabaya katika Michezo ya Olimpiki inayoendelea mjini Rio de Janeiro.

Kenya ililazwa 12-14 na Uhispania katika nusufainali ya Bowl baadaye Jumatano na kupoteza matumaini ya kumaliza angalau nafasi ya tisa na kukamilisha msururu wa matokeo mabaya kwa taifa hilo la Afrika Mashariki mjini Rio.

Awali, walikuwa wameshindwa 7-31 na Japan mechi yao ya mwisho Kundi C siku hiyo ya Jumatano

Shujaa, kama inavyofahamika timu hiyo, walishindwa mechi zote nne walizocheza kufikia sasa.

Walicharazwa 7-31 na Uingereza mechi yao ya ufunguzi na baadaye wakalazwa 5-28 na New Zealand.

Mapema mwaka huu, Kenya ilijipatia matumaini makubwa baada ya kushinda msururu wa mashindano ya raga ya Dunia mjini Singapore.

Sasa, Wakenya hao watashiriki mechi ya kuamua atakayemaliza nafasi ya 11/12 dhidi ya Brazil Alhamisi jioni.