Rwanda yamtimua kocha wa timu ya taifa McKinstry

McKinstry
Image caption McKinstry alikuwa ameongezewa mkataba mapema mwaka huu

Rwanda imemtimua kocha wa timu ya taifa Amavubi, Mwingereza Jonathan McKinstry kwa matokeo yasiyo ya kuridhisha.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya michezo ya Rwanda imethibitisha kuonyeshwa mlango kwa mkufunzi huyo.

Katibu mkuu wa wizara hiyo kanali Patrice Rugambwa amesema sababu ya kumfuta kazi kocha huyo ni matokeo yasiyo ya kuridhisha ya timu ya taifa Amavubi.

Rwanda kwa sasa ni ya tatu katika kundi lake kuwania tiketi ya kufuzu kwa michuano ya Kombe la Afrika la mataifa nchini Gabon mwakani ikiwa na alama 6.

Kundi hili linaongozwa na Ghana, ikifwatiwa na Msumbiji na Mauritius ya mwisho, lakini haina tena matumaini ya kufuzu.

Jonathan McKinstry alipewa mkataba wa kuifundisha Amavubi mwaka jana na ukarefushwa mwaka huu baada ya kuiwezesha kucheza robo fainali ya mashindano ya CHAN ilipoondolewa na DRC.

Alipoanza kuifundisha timu hiyo ilikuwa katika nafasi ya 68 kwa ubora wa FIFA lakini sasa iko kwenye nafasi ya 121.