Kipa Mmarekani aliyesema wapinzani ni waoga aadhibiwa

Hope Solo Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mlinda lango wa timu ya wanawake ya Marekani, Hope Solo

Mlinda lango wa timu ya kina dada ya Marekani, Hope Solo, amepigwa marufuku ya miezi sita na shirikisho la soka la Marekani kwa kuwaita wapinzani wao kutoka Sweden kama 'kundi la watu waoga.' katika michezo ya Olimpiki iliyokamilika hivi majuzi.

Solo mwenye umri wa miaka 35 alisema hayo baada ya timu hiyo ya Sweden kuwatupa nje katika robo fainali, kwa ushindi wa mabao 5-4 kwenye mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare ya 1-1 mjini Rio.

Rais wa shirikisho la soka la Marekani Sunil Gulati amesema matamshi yake 'hayakubaliki'.

Mshindi huyo wa kombe la dunia Solo, kupitia ujumbe wake kwenye mtandao ya kijamii wa Facebook amesema amekasirishwa na uamuzi huo.

Solo hataweza kuchaguliwa kwenye kikosi chake hadi mwezi Februari mwaka ujao.