Ivory Coast kuivaa Tanzania soka ya ufukweni

CAF Haki miliki ya picha CAF

Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu Ufukweni ya Ivory Coast, imo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mpira wa miguu wa ufukweni ambako itacheza na wenyeji Tanzania Ijumaa uwanja Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo utachezeshwa na waamuzi kutoka Uganda ambao ni Shafic Mugerwa atakayepuliza kipyenga na wasaidizi wake ni Ivan Bayige Kintu na Muhammad Ssenteza.

Timu hizo zinatarajiwa kucheza mechi mbili za kuwania kufuzu kwani mara baada ya mchezo wa Dar es Salaam, zitarudiana tena Ivory Coast na mshindi wa jumla atakuwa amefanikiwa kufuzu kwa fainali.

Kwa upande wa Tanzania, Kocha Mkuu wa timu hiyo, John Mwansasu, anaendelea na mazoezi na ameahidi watafanya vizuri katika mchezo huo.

Wanaounda kikosi hicho ni Talib Ame, Ahamada, Mohammed Makame, Ahamed Rajab (golikipa) Khamis Said na Yacob Mohamed wote kutoka Zanzibar.

Wengine ni Ally Raby, Mwalimu Akida, Khalifa Mgaya, Rolland Revocatus, Juma Sultan, Rajab Ghana, Samwel Salonge, Kashiru Salum, Juma Juma na Kevin Baraka.