Shkodran Mustafi na Lucas Perez wakaribia Arsenal

Lucas Perez Martinez Haki miliki ya picha AFP
Image caption Lucas alifunga mabao 17 La Liga msimu uliopita

Mshambuliaji wa Deportivo La Coruna Lucas Perez na beki wa Valencia Shkodran Mustafi wanatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya Arsenal siku ya Ijumaa kabla ya kujiunga na klabu hiyo.

Gunners wamekubaliana na Valencia kuhusu beki wa kati Mustafi, 24, ambaye anatarajiwa kutia saini mkataba wa miaka mitano kwa £35m.

Aidha, wamekubali kutoa euro 20m (£17.1m) kumnunua mshambuliaji wa Deportivo La Coruna Perez, 27, aliyefunga mabao 17 kutoka kwa mechi 37 alizocheza msimu uliopita.

Ununuzi huo utapelekea kiasi cha pesa zilizotumiwa na Arsenal kuwanunua wachezaji kufika £100m tangu kumalizika kwa msimu uliopita.

Klabu hiyo imenunua kiungo wa kati Granit Xhaka, beki Rob Holding, mshambuliaji Takuma Asano na kiungo wa kati Kelechi Nwakali.

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema si kweli kwamba hataki kutumia pesa kuwanunua wachezaji.

Hii ni baada ya kushurumiwa na baadhi ya wachezaji kwamba yeye huwa 'mchoyo sana' sokoni.