Thierry Henry: Nyota wa zamani wa Arsenal apewa kazi Ubelgiji

Thierry Henry
Maelezo ya picha,

Thierry Henry aliacha kazi Arsenal Julai

Meneja wa timu ya taifa ya Ubelgiji Roberto Martinez amesema nyota wa zamani wa klabu za Arsenal na Barcelona, Thierry, ambaye pia aling'aa sana akichezea timu ya taifa ya Ufaransa, atakuwa mmoja wa wasaidizi wake.

Henry alikuwa mmoja wa wakufunzi wa timu ya vijana Arsenal lakini akajiuzulu Julai baada ya meneja Arsene Wenger kumwambia kwamba hawezi kufanya kazi hiyo akiwa bado anaendelea kuwa mchanganuzi wa soka kwenye runinga.

Nyota huyo huchambua soka katika Sky Sports na pia alifanya kazi na BBC Sport wakati wa Euro 2016.

Thierry Henry alikuwa kwenye kikosi cha Ufaransa kilichoshinda Kombe la Dunia mwaka 1998 nyumbani.