Gareth Bale: Sijali kupoteza taji la mchezaji ghali duniani

Gareth bale na Paul Pogba
Image caption Gareth bale na Paul Pogba

Mchezaji wa Real Madrid Gareth Bale anasema kuwa hashtushwi na hatua ya kupoteza taji la kuwa mchezaji ghali zaidi duniani alilopoteza kwa Paul Pogba.

Bale alipoteza taji hilo kwa Pogba baada ya miaka mitatu kufuatia hatua ya mchezaji huyo wa Ufaransa kujiunga na kikosi cha Manchester United kwa kitita cha pauni 89 mwezi uliopita.

Gharama hiyo ya uhamisho iliipita ile ya Bale aliyehamia kutoka Tottenham Hotspurs hadi Real Madrid kwa takriban pauni milioni 85.3.

''Sijali kupoteza taji hilo'',alisema Bale,ambaye yuko na kikosi cha Wales kinachojiandaa kwa mechi ya kufuzu kwa kombe la dunia siku ya Jumatatu nyumbani dhidi ya Moldova.

Huku Wales ikilenga kushiriki katika kombe la dunia la kwanza tangu mwaka 1958,Bale pia anatumai kuwa mchezaji wa sita nchini kwao kushinda kombel la Ulaya pamoja na lile la vilabu bingwa nyumbani.