Mkimbiaji wa Ethiopia Leyisa Lilesa aliyepinga serikali awasili Marekani

Feyisa Lilesa Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ishara ya X inaonyesha upinzani dhidi ya Serikali nchini Ethiopia

Mwanariadha wa Ethiopia na mshindi wa medali ya fedha wa mbio za marathon za Olimpiki Feyisa Lilesa aliyeonyesha alama ya X alipomaliza mbio zake amewasili nchini Marekani.

Hii inatokea takriban wiki tatu baada ya taarifa yake kugonga vichwa vya habari kuhusu alipokunja juu mikono yake kwa alama ya X juu ya kichwa chake wakati akimaliza mbio hizo mjini Rio.

Alama hiyo ni ishara ya kuipinga serikali inayotumiwa na waandamanaji katika jimbo anakotoka la Oromia na imeifanya dunia kutambua wimbi la maandamano ya upinzani nchini Ethiopia.

Bw Feyisa iwapo atarejea nyumbani atakuwa na hofu ya maisha yake ama anaweza kukabiliwa na kifungo cha gerezani kutokana na tendo hilo alilolifanya.

Aliishi nchini Brazil baada ya kushinda medali yake katika siku ya mwisho ya michezo hiyo tarehe 21 Agosti, ambapo alikataa kurejea nyumbani na timu ya wanariadha wengine wa Ethiopia.

Serikali ya Ethiopia ilisema itampokea nyumbani kama shujaa.

Bw Feyisa alisema kuwa ameazimia kuomba uhamiaji nchini Marekani.

Kwa sasa yuko mjini Washington DC baada ya kupewa kibali cha dharura cha kuishi nchini humo.

Ukurara wa mtandao wa kijamii umefunguliwa na waethiopia wanaoishi Marekani kwa ajili ya kutafuta fedha za udhamini wa mahitaji ya maisha yake .

Ndugu na jamaa zake bado wanaishi nchini Ethiopia.