Mo Farah afedheheshwa katika uwanja wa ndege Marekani

Mohammed Farah na familia yake
Image caption Mohammed Farah na familia yake

Mo Farah alifedheheshwa na kurudishwa nyuma ya foleni na muhudumu mmoja wa kampuni moja ya ndege,alipokuwa akisubiri ndege nchini Marekani ,mkewe amesema.

Tania Farah amesema kuwa muhudumu huyo wa kampuni ya ndege ya Delta Airlines alimkaripia mshindi huyo mara nne wa medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki na kukataa kuamini kwamba alikuwa na tiketi aina ya Bussines Class.

''Nilijua kwamba ana matatizo naye'',aliliambia gazeti la Sunday Telegraph.

Msemaji wa Delta Airlines amesema kuwa kampuni hiyo inachunguza tukio hilo na itashirikiana moja kwa moja na familia ya mwanariadha huyo.

Farah ambaye alihifadhi taji lake katika mbio za mita 5,000 na 10,000 katika michezo ya Olimpiki ya Rio pamoja na familia yake walikuwa wakisafiri kutoka Atlanta kuelekea nyumbani kwake huko Partland Oregon.

''Huyu mwanamke alimfedhehesha hadi watu wakajitokeza na kusema huyo ni Mo Farah,bingwa wa Olimpiki'',alisema mkewe.

'Alishtuka baadaye lakini tayari alikuwa amemkaripia.Alikuwa mtu mweusi pekee na hakuwa amefanya chochote cha yeye kufanyiwa alivyofanyiwa'',aliongezea mkewe.