Rogers: Luis Suarez ndiye bora zaidi duniani

Brendan Rodgers, Luis Suarez Haki miliki ya picha Getty Images

Meneja wa klabu ya Celtic ya Scotland Brendan Rogers amesema mchezaji wa klabu ya Barcelona ya Uhispania ndiye mshambuliaji bora zaidi duniani.

Rogers, akizungumza kabla ya mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kati ya klabu hizo mbili baadaye Jumanne amemweleza Suarez kama "mchezaji mtanashati".

"Kwa sasa, Luis ndiye mshambuliaji bora zaidi duniani. Na sidhani kuna swali au shaka kuhusu hilo. Kwanza, ukimzungumzia Suarez ni lazima umzungumzie yeye binafsi. Ni mmoja wa wachezaji watanashati zaidi. Mnyenyekevu. Ana bidii sana. Ni mtu wa familia, ambaye hujitolea kwa hali na mali kwa soka na familia.

"Najivunia kufanya kazi naye kama binadamu kwa miaka miwili, na nilifurahia. Kama mchezaji soka, ndiye bora zaidi."

"Alijiunga na klabu bora zaidi duniani na akawaboresha. Barca haiwezi kuwa ilivyo sasa bila Suarez. Huwa twawasiliana."

Suarez alichezea Liverpool Rogers alipokuwa meneja.

Alihama klabu hiyo mwaka 2014. Mwezi Mei mwaka huu, alimsifu mkufunzi huyo akisema alimsaidia kujiimarisha.

Barcelona walikutana na Celtic hatua ya makundi Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya 2004, 2008, 2012 na 2013.

Haki miliki ya picha EPA

Klabu hizo zilikutana pia Kombe la Fairs 1964 na Kombe la Uefa 2004.

Katika mechi hizo 12, Celtic walishinda mechi mbili pekee, wakatoka sare tatu na kushindwa saba.

Celtic walifanikiwa kulaza Barcelona 2-1 mechi makundi Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya iliyochezewa Parkhead mwaka 2012.

Mkenya Victor Wanyama alifunga bao moja la Celtic dakika ya 21 bao hilo jingine likitoka kwa Tony Watt.