Ligi ya Mabingwa: Paris St-Germain 1-1 Arsenal

Alexis Sanchez Haki miliki ya picha AP
Image caption Arsenal walionekana kutatizwa na washambuliaji wa PSG

Alexis Sanchez aliwasaidia Arsenal kuondoka na alama moja mechi yao ya kwanza msimu huu Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Paris St-Germain.

Edinson Cavani aliwaweka PSG mbele baada ya sekunde 42 pekee na alikuwa na nafasi ya kufunga mabao matatu kufikia muda wa mapumziko.

Alikosa bao wazi baada ya kumchenga David Ospina lakini akatuma kombora lake nje na baadaye kidogo akashindwa kufunga bao rahisi.

Sanchez alifunga bao kwa kutumia vyema mpira uliodunda baada ya Arsenal kupata kombora la kwanza kabisa la kulenga goli.

Alex Iwobi alikuwa na fursa ya kufungia Arsenal bao la ushindi dakika za mwisho lakini akashindwa.

Nyota wa Arsenal Olivier Giroud na Marco Verratti wa PSG walioneshwa kadi nyekundu.

Giroud alikuwa ameingizwa kama nguvu mpya na akajipatia kadi mbili za manjano katika dakika 27, ya pili ikitokana na kisa ambapo alikaripiana na Mwitaliano Verratti ambaye pia alipewa kadi ya pili ya njano.

Gunners walionekana kuzidiwa na kasi ya Cavani, Angel di Maria na Serge Aurier na waliokolewa sana na kipa wa Colombia Ospina ,ambaye alitumiwa langoni badala ya kipa wao nambari wani Petr Cech.

Katika mechi hiyo nyingine ya Kundi A, Waswizi Basel walitoka sare 1-1 nyumbani kwa Ludogorets Razgrad wa Bulgaria.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Ospina na Serge Aurier

Mechi inayofuata kwa Arsenal ni ya Ligi ya Premia dhidi ya Hull saa kumi na moja jioni Jumamosi. Watarejea Ligi ya Mabingwa dhidi ya Basel 28 Septemba, PSG nao wakiwa ugenini Ludogorets.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii