Ligi ya Mabingwa: Club Brugge 0-3 Leicester City

Riyad Mahrez akifunga bao la pili Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Frikiki ya Riyad Mahrez ilipatikana baada ya Jamie Vardy kuangushwa akijibu shambulizi

Leicester City wanasherehekea ushindi wao wa kwanza kabisa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, ushindi mkubwa dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji.

Marc Albrighton alifunga bao la kwanza mara yao ya kwanza kushambulia baada ya kosa la beki wa kulia wa Club Brugge Luis Hernandez.

Riyad Mahrez baadaye alifunga kupitia mkwaju wa adhabu na kufanya mambo kuwa 2-0 kabla ya mapumziko.

Mahrez kisha alifunga kupitia mkwaju wa penalti baada ya Jamie Vardy kuangushwa na kipa wa Brugge.

Jose Izquierdo wa Brugge alikuwa amepata nafasi nzuri lakini akagongesha mpira wake kwenye mlingoti wa goli.

Mabingwa hao wa Ligi ya Premia walionekana kucheza kwa ukomavu mkubwa na kuonyesha wana uwezo wa kushindana katika soka ya Ulaya.

Hiyo ilikuwa mechi yao ya tisa kucheza Ulaya katika historia yao. Aidha, ilikuwa mechi yao ya kwanza kushinda Ulaya tangu ushindi wao dhidi ya Glenavon ya Ireland Kaskazini hatua ya kufuzu kabla ya hatua ya makundi katika Kombe la Wasindi 1961-62, kipa mshindi wa Kombe la Dunia la mwaka 1966 Gordon Banks alipokuwa mlinda lango wao.

Kwenye mechi hiyo nyingine ya Kundi G, FC Porto ya Ureno ilitoka sare 1-1 nyumbani dhidi ya FC Copenhagen ya Denmark.

Haki miliki ya picha @stringersport
Image caption Mashabiki wa Leicester walitengewa tiketi 1,400 pekee mechi hiyo
Haki miliki ya picha Rex Features
Image caption Winga wa Algeria Riyadh Mahrez alifunga mabao mawili

Leicester watarejea uwanjani Ligi ya Premia Jumamosi watakaokuwa wenyeji wa Burnley saa kumi na moja jioni saa za Afrika Mashariki. Watarejea Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Jumanne 27 Septemba, watakapokuwa wenyeji wa FC Porto.