Lyon yakataa kumsajili Adebayor

Emmanuel Adebayor
Image caption Emmanuel Adebayor

Lyon imejiondoa katika juhudi za kumsajili aliyekuwa mshambuliaji wa Arsenal,Manchester City na Tottenham Emmanuel Adebayor.

Adebayor ambaye ni ajenti huru baada kuachiliwa na Crystal Palace alisafiri hadi mjini Lyon na kukutana na kocha Bruno Genesio siku ya Ijumaa.

Lakini klabu hiyo ya Ligue 1 haikufurahishwa na hatua za kumkosa mchezaji huyo kwa miezi miwili ya msimu huu ambapo ataichezea Togo katika kombe la mataifa ya bara Afrika.

Lyon imesema kuwa kushindwa kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 kuiwakilisha Lyon wakati wa mechi za kimakundi za klabu bingwa Ulaya pia ni swala tete.

Vilabu vinafaa kutoa orodha za wachezaji watakaoviwakilisha kufikia Septemba mosi huku mabadiliko yoyote yakikataliwa,hata iwapo mchezaji yupo huru,hadi pale raundi ya muondoano inapoanza.

Lyon ilisema katika taarifa yake kwamba inafurahia kumsajili mshambuliaji mwengine Jean Phillipe Mateta baada ya Adebayor kusema kuwa angependa kuliwakilisha taifa lake katika kombe la bara Afrika mapema 2017, hatua ambayo ingemfanya kutochezea timu hiyo kwa kati ya mwezi mmoja hadi miwili.

Kombe la bara Afrika litafanyika nchini Gabon kati ya Januari 14 hadi Februari 5.