EFL: Chelsea watoka nyuma na kulaza Leicester City

Cesc Fabregas Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ilikuwa mara ya kwanza Cesc Fabregas kufunga msimu huu

Cesc Fabregas alifunga mabao mawili muda wa ziada na kusaidia Chelsea kujikwamua na kulaza Leicester City katika mechi ya raundi ya tatu Kombe la Ligi (EFL).

Leicester walikuwa wamesalia wachezaji 10 wakati wa kumalizika kwa mechi baada ya Marcin Wasilewski kupewa kadi nyekundu dakika ya 89.

Muda mfupi kabla ya mapumziko, Chelsea walikuwa 2-0 nyuma kutokana na mabao ya Shinji Okazaki dakika ya 17 na 34 lakini Gary Cahill alikomboa moja muda mfupi kabla ya kipenga cha mapumziko kupulizwa.

Cesar Azpilicueta alisawazisha kwa kombora la mbali dakika ya 49.

Fabregas, 29, aliwaweka mbele kwa bao alilofunga dakika ya 92 kabla ya kuongeza jingine dakika ya 94.

Wasilewski alioneshwa kadi ya pili ya njano kwa kumgonga kwa kiwiko cha mkono mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kurejea kwa David Luiz hakujawasaidia Chelsea kuziba mianya safu ya ulinzi
Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Fabregas alifunga mabao mawili katika kipindi cha dakika mbili na sekunde 29

Leicester watarejea uwanjani Ligi ya Premia kwa mechi ya ugenini dhidi ya Manchester United Jumamosi.

Chelsea, nao watakuwa ugenini Arsenal siku iyo hiyo baada ya kulazwa 2-1 na Liverpool ligini Ijumaa iliyopita.

MECHI NYINGINE ZA JUMANNE 20 SEPTEMBA 2016

  • Bournemouth 2-3 Preston
  • Brighton 1-2 Reading
  • Derby 0-3 Liverpool
  • Everton 0-2 Norwich
  • Leeds 1-0 Blackburn
  • Leicester 2-4 Chelsea
  • Newcastle 2-0 Wolves
  • Nottm Forest 0-4 Arsenal