Cesc Fabregas amwagiwa sifa na Antonio Conte

Cesc Fabregas asifiwa na mkufunzi Antonio Conte
Image caption Cesc Fabregas asifiwa na mkufunzi Antonio Conte

Meneja wa Chelsea, Antonio Conte amesifu mabao mawili yaliyofungwa na Cesc Fabregas lakini amesisitiza sifa hizo hazimaanishi chochote baada ya kutoka nyuma na kuichapa Leicester City jana.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania alifunga mabao hayo katika muda wa ziada baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 katika muda wa kawaida katika mchezo huo wa mzunguko wa tatu wa Kombe la Ligi na kuwafanya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2.

Fabregas bado hajapata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza katika mchezo wa ligi kuu chini ya Conte huku mchezo pekee mwingine alioanza ukiwa ni ule wa Kombe la Ligi dhidi ya Bristol City mwezi uliopita.

Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Conte amesema anataka ushindi na chaguo la kikosi chake hufanyika ili kupata ushindi na huwa hajali majina yao.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mkufunzi wa Chelsea Antonio Conte

Meneja huyo aliendelea kudai kuwa kwa upande wake jambo muhimu wakati anapomwita mchezaji ni kumuonyesha kuwa hajafanya kosa kufanya hivyo.

Wakati huo huo Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amesema amependa alichokiona kutoka kwa mshambuliaji wake mpya Lucas Perez katika ushindi waliopata katika mchezo wa Kombe la Ligi dhidi ya Nottingham Forest jana.

Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania alifunga mabao yake mawili ya kwanza katika klabu kwenye ushindi wa mabao 4-0 iliyopata Arsenal jana.

Image caption Lucas Perez wa Arsenal

Akihojiwa mara baada ya mchezo huo, Wenger alimsifu mshambuliaji huyo kwa kiwango kikubwa alichoonyesha haswa bao la pili alilofunga.

Wenger amesema bao la pili alilofunga Perez limeonyesha ubora wake kiufundi, nia na morali ya kupambana.