Kina dada wa Chelsea wapewa kichapo na Wolfsburg Stamford Bridge

Zsanett Jakabfi akifunga dhidi ya Chelsea Haki miliki ya picha Rex Features
Image caption Zsanett Jakabfi akifunga dhidi ya Chelsea

Matumaini ya kina dada Chelsea kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya yamefifia baada yao kulazwa 3-0 na kina dada wa Wolfsburg uwanjani Stamford Bridge.

Kiungo wa kati kutoka Hungary Zsanett Jakabfi alifunga mabao yote matatu mechi hiyo na kuiweka klabu hiyo kutoka Ujerumani kwenye nafasi nzuri ya kusonga kutoka hatua ya klabu 32.

Chelsea, ambao kwa sasa wanaongoza ligi kuu ya kina dada Uingereza, walionekana kulemewa kipindi chote cha mechi hiyo iliyotazamwa na mashabiki 3,783.

Wolfsburg, waliofika fainali msimu uliopita, watakuwa wenyeji mechi ya marudiano tarehe 12 Oktoba.

Klabu hiyo imetwaa ubingwa mara mbili tangu msimu wa 2012-13.

Chelsea walishindwa kwa jumla ya mabao 4-1 na Wolfsburg hatua ya klabu 16 bora msimu uliopita.