IAAF yamchunguza Mrusi aliyeshinda Jersey Marathon

Aleksey Troshkin Haki miliki ya picha Jonathan Huelin
Image caption Aleksey Troshkin alimaliza dakika moja mbele ya Mmarekani aliyemaliza wa pili

Shirikisho la Riadha Duniani, IAAF, limeanzisha uchunguzi kubaini iwapo mwanariadha wa Urusi aliyeshinda mbio za Marathon za Jersey alifaa kushiriki mbio hizo.

Hii ni kutokana na marufuku ya kimataifa iliyowekewa wanariadha wa Urusi.

Aleksey Troshkin alishinda mbio hizo kwa mwaka wa tatu mtawalia mapema mwezi huu.

Alikuwa amesalia na sekunde 16 pekee kufikia rekodi yake kwenye mbio hizo.

Lakini wanariadha wa Urusi walipigwa marufuku kushiriki mashindano nje ya taifa lao baada ya kutokea tuhuma za serikali kuunga mkono matumizi ya dawa za kutitimua misuli.

Troshkin huenda akapokonywa taji hilo iwapo itabainika kwamba alikiuka marufuku hiyo.

Mashindano hayo yaliandaliwa Jersey, katika visiwa vya Channel Islands vinavyopatikana baharini kati ya Uingereza na Ufaransa.

Iwapo atapokonywa taji hilo, Mmarekani Chris Zablocki aliyemaliza wa pili atatangazwa mshindi.