Maradona nusura apigane na Veron

Veron akikabilana ana Maradona Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Veron akikabilana ana Maradona

Nguli wa soka nchini Argentina, Diego Maradona na Juan Sebastian Veron siku ya Jumatano nusra wazichape katika mchezo wa hisani uliofanyika jijini Rome, Italia.

Wawili hao walikuwa wakibadilishana maneno mpaka kufikia hatua ya kutaka kushikana wakati wakielekea nje ya uwanja wakati wa mapumziko.

Mchezo mahsusi kwa ajili ya kuhamasisha amani ulioandaliwa na Papa Francis ulihusisha nyota kadhaa waliostaafu na ambao bado wanacheza akiwemo Ronaldinho, Francesco Totti, Edgar Davids, Hernan Crespo na Bojan Krkic.

Kisa cha sakata hilo ni Maradona kuonyeshwa kutofurahishwa na jinsi Veron alivyokuwa akimchezea ambapo ilibidi azuiwe na beki wa zamani wa kimataifa wa Brazil Cafu pamoja na watu wa usalama wakati akitaka kwenda kumvaa Veron.