Kombe la dunia la 2026 huenda likashirikisha timu 46

Ujerumani ndio washindi wa kombe la dunia 2014 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ujerumani ndio washindi wa kombe la dunia 2014

Kombe la dunia linaweza kushirikisha mataifa 40 ama hata 48 baada ya shirikisho la soka duniani Fifa kuwa na ombi la kuongeza idadi ya timu kutoka 32.

Mapendekezo hayo yatatolewa katika makao makuu ya Fifa wakati wa mkutano ujao utakaofanyika tarehe 9 mwezi Januari mwaka 2017.

''Hisia zinazotolewa na wanachma wa baraza ni kwamba zinaunga mkono upanuzi'',alisema rais wa Fifa Gianni Infantino.

Mwandalizi wa dimba hilo mwaka 2026 bado hajatajwa ,huku kombe la dunia la mwaka 2018 likifanyika Urusi na lile la mwaka 2022 likipangiwa kufanyika Qatar.

Infantino alichukua uongozi wa Fifa mnamo mwezi Februari na ahadi zake wakati wa uchaguzi ilikuwa kuongeza idadi ya timu katika dimba la dunia hadi 40.

Hatahivyo mapema mwezi huu raia huyo wa Italy mwenye umri wa miaka 46 alipendekeza kuongeza idadi hiyo hadi 48,huku timu 32 zikishiriki katika awamu ya raundi ya muondoano katika taifa linaloandaa na baadaye washindi kujiunga na timu nyengine 16 katika makundi.

Hatahivyo wakosoaji wa mpango huo wamesema kuwa utadhoofisha ubora wa soka katika fainali hizo.