Real Madrid yaicharaza Real Betis 6-1

Cristiano Ronaldo akifunga bao lake dhidi ya Real Betis Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Cristiano Ronaldo akifunga bao lake dhidi ya Real Betis

Klabu ya Uhispania Real Madrid imeongeza presha kwa wapinzani wake Atletico Madrid katika kilele cha jedwali la ligi ya La Liga baada ya kurekodi ushindi mkubwa dhidi ya Real Betis.

Isco alifunga mabao mawili huku bao la nne la Cristiano Ronaldo msimu huu likiisaidia timu hiyo ya Zinedine Zidane baada ya kupata droo nne mfululizo.

Raphael Varane alifunga kwa kichwa na kuiweka Real kifua mbele kabla ya Karim Benzema kufunga akiwa karibu na lango naye Marcelo akampiga kanzu kipa wa Betis katika kipindi cha kwanza cha mechi.

Bao la Alvaro Cejudo liliipatia Betis matumaini kwa mda kabla ya Isco na Ronaldo kutikisa wavu.

Ushindi huo unamaanisha Real wako pointi 18 sawa na viongozi wa ligi hiyo Atletico ambao wako mbele kwa wingi wa mabao.