Sanches amshinda Rashford tuzo ya mchezaji bora chipukizi Ulaya

Renato Sanches Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Sanches alichezea Ureno mara sita Euro 2016, na kuwafungia bao moja

Kiungo wa kati wa Bayern Munich Renato Sanches amemshinda mshambuliaji wa Manchester United Marcus Rashfordna kushinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi Ulaya.

Sanches, 19, amewafuata Wayne Rooney, Raheem Sterling, Lionel Messi na Sergio Aguero katika kushinda tuzo hiyo ambayo kwa Kiingereza hufahamika kama Golden Boy na hutunukiwa mchezaji bora Ulaya wa chini ya miaka 21.

Rashford na mchezaji mwenzake Sanches Bayern Munich Kingsley Coman walikuwa wanapigania tuzo hiyo na Sanches.

Nyota huyo atakabidhiwa tuzo hiyo katika hafla itakayofanyika Monte Carlo Jumatatu.

Haki miliki ya picha Tuttosport
Image caption Wanahabari kutoka vyombo 30 vya habari Ulaya hupiga kura. Tuzo hiyo hudhaminiwa na gazeti la Italia la Tuttosport

Tuzo hiyo ilianzishwa na gazeti la Tuttosport mwaka 2003.

Sanches alijiunga na Bayern Munich majira ya joto mwaka huu kwa £27.5m na amewachezea mechi nane msimu huu.

Amechezea Ureno mechi 11.

Alicheza Euro 2016 akiwa na miaka 18 na kuwa mchezaji wa umri mdogo zaidi kuchezea timu iliyoshinda.

Aidha, alishinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi katika michuano hiyo.