Mkenya Mary Keitany ashinda Marathon New York

Mary Keitany Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mary Keitany (3), Mwingereza Paula Radcliffe (3) na raia wa Norway Grete Waitz (5) ndio wanawake pekee walioshinda Marathon ya New York mara tatu au zaidi

Mkenya Mary Keitany amekuwa mwanamke wa kwanza kushinda mbio za Marathon za jiji la New York mara tatu mtawalia katika kipindi cha miaka 30.

Keitany, 34, alitumia muda wa saa mbili, dakika 24 na sekunde 26 na kuwa mwanamke wa kwanza kufanya hivyo tangu raia wa Norway Grete Waitz - aliyeshinda mbio hizo mara tano mtawalia.

"Kushinda mara tatu si rahisi, na ina maana kubwa sana kwangu. Si rahisi lakini nilifanikiwa," amesema.

Bingwa wa dunia kutoka Eritrea Ghirmay Ghebreslassie, 20, alimshinda Mkenya Lucas Rotich mbio za wanaume na kuwa mshindi wa Marathon ya New York mwenye umri mdogo zaidi.

Ghebreslassie, aliyemaliza nambari nne London Marathon na Olimpiki Rio alitumia muda wa 2:07:51 na kuwanyima Wakenya ubingwa wa nne mtawalia katika Marathon kwa wanawake na wanaume.

"Najionea fahari sana kutokana na ushindi wangu, na kwamba mimi ni wa kwanza kutoka nchi yangu kushinda," amesema.

Mmarekani Tatyana McFadden alishinda taji lake la nne mbio za wanawake wa kutumia magurudumu New York akitumia muda wa saa moja dakika 47 na sekunde 43.

Sasa ameshinda mbio 17 kubwa za marathon zilizofanyika karibuni, zikiwemo London, Boston, Chicago na New York.