Mexico wawashinda Marekani mechi ya kufuzu kombe la dunia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Nahodha wa Mexico Rafael Marquez (kushoto) akisherehekea na wenzake baada ya kufunga

Nahodha Rafael Marquez alifunga mnamo dakika ya 89 na kuipa Mexico ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Marekani wakati wa mechi ya kufuzu kwa kombe la dunia mwaka 2018.

Mechi hiyo iliyoandaliwa mjini Columbus jimbo la Ohio, inachezwa baada ya Donald Trump kupata ushindi kwenye uchaguzi wa urais nchini Marekani na baada wa kuwakosoa vikali raia wa Mexico kwenye kampeni yake.

Mexico walitangulia kufunga kupitia Miguel Layun kabla ya Marekani kusawazisha kupitia kwa Bobby Wood.

Trump aliwataja wahamiaji kutoka Mexico walio nchini Marekani kuwa wahalifu na kusema kuwa anataka kujenga ukuta kati ya marekani na Mexico.

"Ni muda tangu tuwe na mchezo mzuri hapa. Tuna furaha sana na hili ni jambo muhimu kwetu."alisema Marquez.

Nchi hizo mbilo ziko kundi la timu sita ambapo timu tatu za kwanza zitafuzu kwa mashindano ya kombe la dunia nchini Urusi.

Marekani itacheza mechi yake ya pili dhidi ya Costa Rica siku ya Jumanne huku Mexico ikikutana na Panama.

Mada zinazohusiana