AFOTY: Wasifu wa Pierre-Emerick Aubameyang

Huwezi kusikiliza tena
Pierre-Emerick Aubameyang

Tangu alipoanza kucheza, mshambuliaji huyu wa Borussia Dortmund, mzaliwa wa Gabon alishamiri.

Mgombeaji huyo wa tuzo ya mchezaji bora wa BBC mwaka 2016 mwenye umri wa miaka 27, alikulia nchini Ufaransa.

Alisajiliwa kama mchezaji wa AC Milan ya Italia ambayo hata hivyo hakuichezea kwani alipelekwa kwa mkopo katika timu ya Dijon ya Ufaransa.

Na katika mechi yake ya kwanza ya kirafiki kabla ya msimu kuanza, kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 18 aliwashtua wakubwa zake.

"Unapocheza mechi hiyo ya kwanza ya msimu unakua bado hauko tayari, lakini hata hivyo yeye tayari alikuwa bora na mwepesi kuliko wengine," anasema Flirent Perraud, ambaye wakati huo alikuwa mlinda lango wa timu ya Dijon.

"Uwanjani, tulikuwa tukisema, 'kijana huyu ni nani? ni mchezaji wa ajabu tuliyepewa'.

"Tuligundua kwamba kumbe siyo mtoto mdogo bali mchezaji wa ajabu."

Katika msimu wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa Aubameyang alifunga magoli 10.

Halafu kijana huyo aliyekulia Ufaransa akaanza ziara ya kufana iliyompeleka Colombia, Italia na Mexico (akimfuata mwanasoka Babake Pierre) na wakati huo alihamishwa kwa mkopo katika timu za Lille, Monaco na St Etienne iliyompa mkataba wa kudumu mwaka 2011 na ambapo mchezo wake ulianza kuimarika.

Kutoka huko, kuhamia kwake katika timu ya Dortmund mwaka 2013 kuliharakisha mwendo wake wa kuwa mmoja kati ya washambuliaji wazuri duniani.

Mwezi Juni mwaka 2016 alikuwa Mwafrika wa kwanza kupewa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa ligi kuu ya soka ya Ujerumani - Bundesliga - kufuatia kura inayopigwa na wachezaji wenzake.

Fomu yake pia ilimwezesha 'Auba' kama mchezaji wa kwanza raia wa Gabon kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Afrika ya CAF, na kuwekwa kwenye orodha ndogo ya FIFA ya kuwania kuwa mchezaji bora wa mwaka 2016.

Kimsingi anafahamika kwa upachikaji wake wa magoli.

Ameshanusa nyavu mara 11 katika mechi 9 za Bundesliga, yakiwemo magoli 4 aliyofunga waliposhinda Hamburg 5-2 .

Kwa ujumla ameshaifungia Dortmund magoli 89 katika mechi 152.

Kuna pia kasi yake ambayo ni kubwa ukilinganisha na Usain Bolt katika masafa mafupi, bila kusahau namna yake ya kusherehekea baada ya kufunga goli, mfano wa Batman na Spiderman.

"Anapenda utani na kuchekesha watu, ni kijana mcheshi, rafiki mzuri kabisa," anasema Jordan Loties waliyecheza pamoja katika timu ya Dijon.

Mitindo ya mavazi na nywele zake inaonyesha kwamba kweli Aubameyang ni mtu wa kuvutia ijapokuwa mwenyewe anajieleza kama mwenye kuona haya.

"Nilifanya kazi kwa bidii kufikia kiwango hiki," Aubameyang aliambia BBC.

Mwanasoka kijana, aliyebuni viwanja mfano katika chumba chake kabla ya kuwakilisha timu ya vijana ya Ufaransa, Aubameyang alifuata nyayo za Babake kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Gabon maarufu 'Chui'

"Nilichagua Gabon ili kuiwakilisha Afrika na kuchukua nafasi ya Didier Drogba na Samuel Eto'o," alisema.

"Lakini kufanya hivyo, huna budi kushinda tuzo."

Tayari ana msururu wa tuzo, je tuzo ya BBC itaongezeka katika kabati lake la vikombe?

Piga kura hapa : bbc.com/africanfootball

Mada zinazohusiana