AFOTY: Wasifu wa Andre Ayew

Huwezi kusikiliza tena
Andre Ayew, nyota wa West Ham

Mchezaji wa kimataifa wa Ghana Andre Ayew ameonyesha kwamba siyo mtu wa kuogopa matatizo.

Mwezi wa kwanza, kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 alilazimishwa kucheza katika nafasi isiyokuwa yake wakati Francisco Gidolin alipoanza kuifunza timu ya Swansea baada ya Garry Monk kutimuliwa, na aliidhibiti vizuri sana.

Mtazamo wake chanya na mwendelezo wa kucheza vizuri na kufunga magoli siyo tu ulimsaidia yeye binafsi bali pia uliisaidia timu yake katika kupambana isishuke kutoka ligi kuu ya Uingereza.

Ayew alifunga magoli 2 walipoishinda Liverpool 3-1 na kusaidia timu ya Swansea kupata matokeo mazuri ambayo hatimaye yalithibitisha kusalimika kwake baada ya kampeni iliyokuwa ngumu.

Kwa hivyo siyo jambo la kushangaza kuona kwamba alishinda tuzo ya klabu hiyo ya mchezaji mgeni wa mwaka baada ya msimu.

Fomu yake ilikuwa ya kuvutia kiasi kwamba, mwezi Agosti timu ya West Ham ya mashariki ya jiji la London ilivunja rekodi yake kwa kumsajili Ayew kwa kitita cha pauni milioni 20.5.

Ayew hakuwa na bahati kwani alijeruhiwa vibaya katika mechi yake ya kwanza akiichezea Hammers lakini kadiri atakavyoshiriki mechi nyingi hakuna shaka atathibitisha ada ya uhamisho wake.

Baada ya miezi miwili ya kukosekana kwake alirejea uwanjani mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Na "machoni anaonekana mwenye uchu" kama alivyoona mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ghana Yaw Preko mara ya kwanza walipocheza pamoja na kuwa ndicho kitakachomsaidia kudhihirisha thamani yake kwa timu yake mpya msimu ujao.

Wakati huo huo, kimataifa Ayew ameendelea kuwa mchezaji muhimu kwa timu ya taifa ya Ghana mwaka 2016.

Alikuwa miongoni mwa wafungaji Ghana ilipoilaza Mauritius 2-0 na kutangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo ambapo Black Stars walijikatia tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika mwakani nchini Gabon.

Na kulipokuwa na kipindi kigumu mwaka 2016 cha majeraha na matatizo mengine ya timu, Ayew alijituma kama kawaida yake.

Lakini katika maisha yake Ayew ni mtu aliyezoea kukabiliana na presha na matarajio ya wengi kwa kuwa mtoto wa gwiji wa zamani wa Ghana, Abedi Pele Ayew ambaye anachukuliwa kuwa mmojawapo wa wachezaji bora wa Afrika wakati wote.

Babake Ayew aliichezea Black Stars mara 73 na kufunga magoli 33 huku akiisaidia kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1982 na kunyakua nafasi ya pili mwaka 1992.Pia mwaka 1993 alishinda kombe la klabu bingwa Ulaya akichezea Marseille.

Miaka miwili kabla alikuwa amepoteza fainali ya kombe la Ulaya.

Mengi ya kusisimua sasa

Lakini Ahmed Brynes, mkufunzi wa Nania FC ya Ghana ambako Ayew alianzia kufuata nyayo za babake alitoa ubashiri wake wa kuvutia.

"Ayew alipokuwa tu na umri wa miaka 14, alikuwa mchezaji wa ajabu na tena alikuwa akisema 'nataka kuwa bora zaidi kuliko babangu," Brynes aliambia BBC.

"Nilimwambia,'angalia babako alifika kiwango cha juu sana kuliko wewe'....lakini akajibu 'nitampita' na nina uhakika atapita kiwango hicho."

Abedi Pele Ayew alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mwaka 1992.

Kijana wake Ayew akaiga mfano wake mwaka 2011-Je, mwaka huu ndio unaweza kuwa wa kumpita?

Piga kura hapa : bbc.com/africanfootball

Mada zinazohusiana