AFOTY: Wasifu wa Sadio Mane

Huwezi kusikiliza tena
Sadio Mane, nyota wa Liverpool

Mchezaji soka wa kimataifa wa taifa la Senegal Sadio Mane amekuwa na mwaka wa mafanikio.

Mshambuliaji huyo mwenye kasi anaweza kucheza safu yoyote ya mashambulizi, katika wingi, katikati na hata mbele, na ameonekana kuwa mmoja ya wachezaji hatari katika ligi ya Uingereza mbali na kuwa mmoja ya wachezaji walio na nyota inayong'aa barani Afrika.

Kasi yake, vile anavyodhibiti mpira mbali na anavyofikiria kwa haraka ni suala ambalo huzua hofu miongoni mwa wapinzani wake hatua ambayo imemfanya kuvutia nyoyo za mashabiki na kupata sifa kutoka kwa wataalamu wa soka.

Ni mchezaji mwenye ujanja mwingi sana na ambaye ni mwepesi mbele ya lango mbali na kuweza kuchukua pasi na kutengeza nafasi kwa wachezaji wenza.

Mady Toure, mwanzilishi wa Academie Generation foot, ambapo Mane alianza elimu yake ya soka, anaamini kuwa Mane ni mchezaji aliyetimia.

"Sadio Mane ana kitu ambacho hata Lionel Messi hana, kitu ambacho hata Neymar hana," aliambia BBC michezo.

Mane alimaliza msimu uliopita akiwa mfungaji bora wa Southampton akiongoza na mabao 15 katika mashindano yote na akafanikiwa kupata uhamisho kwenda Liverpool kwa kitita cha pauni milioni 34.

Uhamisho huo hadi Liverpool ulimfanya kuwa mchezaji ghali zaidi wa Afrika katika historia, huku fedha za uhamisho wake zipiku zile ambazo klabu ya Manchester City iliilipa Swansea ili kumnunua mshambuliaji Wilfried Bony mnamo mwezi Januari 2015.

Mane ana mabao sita na amsaidia ufungaji wa mabao 11 kwa Liverpool msimu huu.

Amekuwa aking'ara tangu ajiunge na Liverpool, ambapo alifunga katika mechi yake ya kwanza na Liverpool katika ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Arsenal katika mechi ya ufunguzi wa msimu.

Mane alionyesha umahiri wake tena kwa kufunga bao moja huku akitengeza jingine katika mechi iliofuata, na mechi nyengine Mane alitengeneza nafasi mbili za mabao huku Liverpool ikiicharaza Burton Albion 5-0 katika mechi ya kombe la ligi.

Alithibitisha uwezo wake katika kufunga mabao kwa kufunga bao moja na kusaidia ufungaji wa jingine katika ushindi wa nyumbani wa 4-1 dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi, Leicester mbele ya mashabiki wao.

Mabao yake mengine yalitokana na mechi za ligi katika ushindi dhidi ya Hull City na West Brom na hivi karibuni alifunga mabao mawili katika ushindi wa 6-1 dhidi ya Watford.

Katika safu ya kimataifa, Mane alikuwa nyota wa Senegal katika mechi ya ufunguzi wa kufuzu katika kombe la dunia la mwaka 2018 mnamo mwezi Oktoba, akithibitisha kuwa mchezaji muhimu na vilevile akafanikiwa kufunga bao muhimu katika mechi dhidi ya Cape Verde.

Akiwa amechezeshwa mara 36 na taifa lake, Mane anajivunia mabao 10 na kutoa usaidizi wa mabao 11 kwa timu ya Simba wa Teranga na atakuwa kiungo muhimu katika matumaini yao ya kufuzu kwenda Urusi 2018 pamoja na Kombe la Taifa Bingwa Afrika mwakani nchini Gabon

Mchezo wa Mane katika klabu yake na taifa umemfanya kuwa na thamani kubwa katika orodha ya mgombea wa mchezaji bora wa BBC wa mwaka, kwa mwaka wa pili mfululizo.

Tayari uamuzi wake wa kuacha shule akiwa umri wa miaka 15 na kuanza kucheza soka ya kulipwa umempatia ufanisi mkubwa.

Alishinda taji la ligi na lile la kombe la ligi mara mbili akiichezea timu ya FC Salzburg ya Austria 2014 .

Ni mshambuliaji wa Senegal anayetegemewa sana na mnamo mwezi Mei 2015 aliweka rekodi mpya ya kufunga mabao matatu kwa haraka katika historia ya ligi hiyo wakati alipofunga hatrick (mabao matatu mechi moja) katika sekunde 175 akiichezea Southampton dhidi ya Aston Villa.

Akianza soka yake huko Sidhiou hadi katika ligi ya Uingereza kupitia Dakar, Ufaransa na Austria safari ya Mane imejaa bashasha.

Na ukweli ni kwamba ana uwezo wa kuwa mchezaji bora wa Afrika atakayeenziwa.

Piga kura hapa : bbc.com/africanfootball

Mada zinazohusiana