Mikel aashiria huenda akaihama Chelsea

Obi Mikel Haki miliki ya picha Getty Images

Kiungo wa kati wa Chelsea John Mikel Obi amedokeza kwamba huenda akaihama klabu hiyo ya ligi ya Premia kipindi kifupi cha kuhama wachezaji mwezi Januari.

Mikel mwenye umri wa miaka 29, amekuwa na timu hiyo ya Blues kwa miaka 10, na ni mchezaji wa pili ambaye amehudumu kwenye klabu kwa muda mrefu nyuma ya nahodha John Terry, lakini bado hajachezeshwa msimu huu.

''Nitaendelea kufanya vyema, na kuwa tayari ninapohitajika,"amesema Mikel.

"Tutaona kitakachotokea mwezi Januari.''

Kocha wa timu ya taifa ya Nigeria Gernot Rohr, amesema Mikel aliadhibiwa kwa kuiwakilisha nchi yake kwa michezo ya Olimpiki Rio kabla ya msimu kuanza.

Mikel alipokuwa nahodha, Nigeria ilishinda medali ya shaba katika michezo nchini Brazil na alisema medali hiyo ni kitu ambacho ''hawezi kukibadilisha na kitu chochote.''

Tangu kuwasili kwake katika uwanja wa Stamford Bridge mwaka 2006, kwa pauni milioni 16, Mikel ameisaidia timu yake kushinda taji kuu la Premia mara mbili, kombe la FA mara nne, kombe la ubingwa barani ulaya na ligi ya bara Ulaya.

Hata hivyo, hajabahatika kucheza msimu huu chini ya uongozi mpya wa meneja Antonio Conte.

''Mimi si mtu wa kutafuta sababu maishani mwangu, sitayaonea haya majukumu yangu,"Mikel aliiambia BBC.

''Nitajaribu kufanya bidii zaidi ili nihakikishe nimebadilisha mawazo ya Meneja Conte. Nimekuwa nikifanya mazoezi na timu hiyo natumai siku moja nitashirikishwa kwenye mchezo.''