Manchester City na Chelsea washtakiwa na FA

Manchester City v Chelsea Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wachezaji na maafisa wa klabu zote mbili walihusika katika mtafaruku huo

Klabu za Manchester City na Chelsea zimeshtakiwa na FA kwa kushindwa kuwadhibiti wachezaji wakati wa mechi ya Ligi ya Premia iliyochezwa Jumamosi.

Mashtaka hayo yanatokana na mfarakano wa wachezaji uliozuka dakika ya 95 wakati wa mechi hiyo iliyochezewa Etihad ambapo Chelsea walishinda 3-1.

Mshambuliaji wa City Sergio Aguero na kiungo wa kati Fernandinho walifukuzwa uwanjani, lakini kiungo wa kati wa Chelsea Cesc Fabregas hatachukuliwa hatua.

Meneja wa City Pep Guardiola aliomba radhi kwa mchango wa timu yake katika kisa hicho.

Aguero, 28, amepigwa marufuku kucheza mechi nne kutokana na kisa chake hicho cha pili cha kufukuzwa uwanjani kwa utovu wa nidhamu, baada yake kumkabili visivyo beki wa Chelsea David Luiz.

Fernandinho walikabiliana na Fabregas baada ya kosa hilo la Aguero, na Mbrazil huyo atatumikia marufuku ya mechi tatu.

Klabu zote zimepewa hadi saa 18:00 GMT mnamo 8 Desemba kujibu mashtaka hayo.

Mada zinazohusiana