Barcelona kushiriki mechi ya kirafiki na Chapecoense mwaka 2017

Wachezaji wa Chapecoense Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wachezaji wa Chapecoense

Barcelona wameikarabisha klabu ya Brazil ya Chapecoense kwa mechi ya kirafiki kabla msimu wa kiangazi ujao.

Wachezaji 19 wa Chapecoense na wahudumu wa klabu hiyo walikuwa miongoni mwa watu 71 waliuawa katika ajali ya ndege iliyokuwa ikiwasafirisha kutoka Colombia kwa michuano ya fainali ya mkondo wa kwanza wa Sudamericana.

Mechi hiyo ya kirafiki itakuwa ya kuwania kombe la Joan Gamper, ambayo huandaliwa kila mwaka kati ya klabu ya Barcelona na timu alikwa.

Katika taarifa, Barcelona imesema walitaka ''kutoa heshima zao za mwisho'' kwa waathiriwa na kuisaidia timu ya Chapecoense kustawi tena.

Wachezaji watatu wa Chapecoense walikuwa miongoni mwa watu sita walinusurika katika mkasa huo.

Barcelona wamesema walitaka kulifanya kombe hilo la Joan Gamper kama 'heshima yao kubwa kwa ulimwengu wa soka kupitia shughuli mbalimbali zitakazo andaliwa kwenye mchuano huo.

''Licha ya kuialika timu hiyo ya Chapecoense kwa kombe la Joan Gamper mwaka 2017, Barcelona pia wamesema wangependa kushirikiana na klabu hiyo kwa ujenzi wa uwanja ili kuisaidia timu hiyo kujiendeleza katika kiwango cha ushindani waliokuwa nao hapo awali,''waliongezea Barcelona.

Barcelona leo hii imetuma barua rasmi ya mualiko kwa bodi ya wakurungezi wa klabu ya Chapecoense.