Mane na Mahrez kushindania tuzo kuu ya BBC Afrika

Mahrez na Mane

Riyad Mahrez wa Algeria na Sadio Mane wa Senegal, mmoja wao atatawazwa Mwanakandanda Bora wa Afrika wa mwaka 2016 baadaye Jumatatu.

Mashabiki kutoka pande mbalimbali duniani walipigia mchezaji wanayetaka ashinde tuzo hii mwaka 2016.

Orodha ya awali ya wachezaji watano inapunguzwa, bila kufuata utaratibu wwote, na Pierre-Emerick Aubameyang, Andre Ayew na Yaya Toure waliondolewa mapema Jumatatu.

Mshindi atatangazwa moja kwa moja katika runinga na redio ya BBC Focus on Africa na mtandaoni saa 17:45 GMT (saa tatu kasorobo Afrika Mashariki).

Ni mara ya kwanza kwa mshambuliaji wa Leicester na Algeria Mahrez kuteuliwa kushindania tuzo hii.

Mchezaji huyu wa umri wa miaka 25 alifana sana na kuisaidia klabu yake ya Ligi ya Premia, ambayo ilipewa uwezekano wa kushinda mwanzoni mwa msimu kuwa 5000-1 pekee, kushinda taji lao la kwanza la ligi.

Alifunga mabao 17 ligini na pia alichaguliwa Mchezaji Bora wa Mwaka Uingereza na wachezaji wenzake - mwafrika wa kwanza kushinda tuzo hiyo. Aidha, aling'aa akichezea Algeria na kuwasaidia kufuzu kwa Kombe la Taifa Bingwa Afrika mwaka 2017.

Mshambuliaji wa Senegal Mane, 24, aliibuka mchezaji ghali zaidi Mwafrika katika historia alipojiunga na Liverpool kwa £34m majira ya joto.

Amechangia sana uchezaji Anfield, ambapo amewafungia mabao saba katika mechi 15. Kabla ya kuhama kwake, alifunga mabao manane ligini mwaka huu akichezea Southampton, yakiwemo mabao matatu mechi moja dhidi ya mabingwa wa wakati huo Manchester City.

Mshindi atajiunga na kundi la wachezaji mashuhuri Afrika ambao wameshinda tuzo hiyo awali, wakiwemo Dider Drogba, Mohamed Aboutrika na Jay-Jay Okocha.

Mada zinazohusiana