Uganda haikuweza kulipia leseni ya matangazo AFCON

Mashabiki wa timu ya taifa ya Uganda, Cranes Novemba 12, 2016 Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Mashabiki wa timu ya taifa ya Uganda, Cranes

Shirika la Utangazaji la Uganda (UBC) limesema halikufanikiwa kupata haki ya kupeperusha mechi za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) moja kwa moja kutokana na uhaba wa pesa.

Hii ni licha ya kwamba timu ya taifa ya Uganda, Cranes, inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.

UBC imesema haikuweza kupata $600,00 ( £485, 000) zinazohitajika kujipatia leseni ya kupeperusha mechi hizo.

Badala yake, shirika hilo litawatangazia raia wa Uganda matukio makuu pekee kwenye mechi.

"Ni kwa masikitiko makubwa ambapo tunawatangazia rasmi watazamaji wetu na taifa kwa jumla kwamba UBC itapeperusha tu matukio makuu ya mechi na kutoa matangazo ya redio pekee kupitia vituo vyetu vyote," taarifa ya UBC imesema.

Mwandishi wa BBC nchini Uganda Catherine Byaruhanga anasema kuna uwezekano kwamba serikali itaingilia kati kusaidia, kama ilivyofanya mara kadha awali.

Kiongozi wa upinzani Kizza Besiye amesema ni aibu kubwa kwamba UBC haiwezi kununua haki za kupeperusha mechi za michuano hiyo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii