Klabu ya China yazuiwa kumnunua Costa kutoka Chelsea

Diego Costa Haki miliki ya picha Rex Features

Mpango wa klabu ya China ya Tianjin Quanjian kumsajili Diego Costa kutoka Chelsea umegonga mwamba kutokana na sheria mpya iliyotolewa kwa klabu zinazocheza ligi kuu ya China, amesema mmiliki wa klabu hiyo Shu Yuhui.

Shu anadai Tianjin ilikuwa na mipango ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil Costa, 28, na washambuliaji Karim Benzema, Radamel Falcao and Edinson Cavani

Lakini klabu za Uchina zitaruhusiwa kuwachezesha wachezaji watatu pekee wa kutoka nchi za nje, msimu ujao unapoanza kwa mujibu wa sheria mpya.

''Hali hiyo imesababisha mabadiliko katika mipango ya kuwasajili wachezaji,''amesema Shu.

Klabu hapo awali zilikuwa zikiwatetua wachezaji wanne kutoka taifa lolote na raia mmoja kutoka Asia katika kikosi chao.

Kutoka mwanzo wa msimu mpya, mwezi Machi, lazima wa wajumuishe wachezaji wawili wa Uchina wenye umri wa chini ya miaka 23 kwenye kikosi cha kucheza mechi, na mmoja anastahili kuwa miongoni mwa wachezaji 11 wa kuanza mechi.

Shu amesema Tianjin ingekuwa imefanya 'uwekezaji mkubwa' mwaka huu iwapo sheria za hapo awali zingesalia.

Akizungumza na runinga ya Tianjin, Shu amesema mikataba ilikuwa imekubaliwa kwa mshambuliaji wa Monaco Radamel Falcao,30, na mshambuliaji wa Benfica Raul Jimenez, 25, kabla ya sheria hiyo mpya kupitishwa siku ya Jumatatu .

Costa amehusishwa na kuihamia China kwa pauni milioni 30 kwa mwaka, ingawaje Chelsea haikuwa na mpango wa kumuuza.

Bilionea Shu ameongezea kuwa Costa na Cavani,29, wangekuwa wametia saini mikataba kufikia sasa lakini klabu zao hazikutaka wahame wakati msimu wa soka Ulaya bado unaendelea.

Tiajin ilipandishwa ngazi kucheza Ligi Kuu ya China uliopita na meneja wao ni Mtaliano mshindi wa Kombe la Dunia Fabio Cannavaro.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii