Kundi la Urusi ladukua mtandao wa CAF

Ali Bongo na Issa Hayatou Haki miliki ya picha Gabriel Bouys
Image caption Rais wa Gabon Ali Bongo na rais wa Caf Issa Hayatou nchini Gabon

Shirikisho la soka barani Afrika limechukua hatua ya kuulinda mtandao wake baada ya kubainika ulikuwa umedukuliwa.

Kundi mmoja la Urusi la New World Hackers, linadai lilidukuwa mtandao huo.

Wanachama wa kundi hilo waliiambia BBC kwamba walifanya hivyo 'kupinga' Gabon, mwenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

''Gabon ni nchi ya udikteta,'' mwanachama mmoja wa kundi hilo ameiambia BBC Sports.

Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) limeongeza shughuli ya sekunde tano ya kuwachunguza wageni wote kwenye mtandao wake, ifahamikayo kama Cloudflare, kama njia ya kukabiliana na shida hiyo.

"CAF imechukua hatua lakini hatuwezi kusema kwa asilimia 100 kwamba kisa kama hicho hakitatokea tena,'' Junior Binyam, mkurugezi wa maswala ya mawasiliano wa shirikisho hilo amesema.

''Hata Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) liliwahi kudukuliwa.''

Mtandao wa CAF ulifungwa kwa saa tano siku ya Jumamosi, na kusababisha viongozi wa bodi hiyo kuchunguza hitalafu ya kimtandao wakidhani ilikuwa chanzo, kabla ya kubaini tatizo lilitokana na udukuzi

Mwaka huu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika imepingwa na raia kadhaa wa Gabon ambao wametumia nafasi hiyo kuelezea malalamiko yao ya kisiasa.

Haki miliki ya picha Gabriel Bouys
Image caption Mashabiki wa Gabon

Maafisa wa Gabon wamesema watu watatu waliuawa kutokana na makabiliano makali ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwaka jana.

Upinzani ukiongozwa na mwenyekiti wa zamani wa tume ya Umoja wa Afrika Jean Ping umesema idadi ya waliofariki ilikuwa juu.

Miezi iliyofuata upinzani uliwataka raia kususia michuano ya soka iliyoanza rasmi tarehe 14 Januari na inatarajiwa kukamilika Februari 5 .

Siku ya Jumapili New World Hackers, pia walidai kudukua mtandao wa kampuni ya mafuta ya Total, ambayo ilitangaza udhamini mkubwa wa mamilioni ya dola kwa CAF mwaka jana.

BBC imejaribu kuwasiliana na kampuni hiyo ya Total lakini hawajasema lolote.

Gabon imekuwa timu ya kwanza kati ya 23 zilizoadhimisha kombe la afrika kubaduliwa nje katika hatua ya makundi walipotoka sare na Cameroon.

Mada zinazohusiana