Arsenal walaza Sutton na kutua robo fainali Kombe la FA

Lucas Perez

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Perez sasa amehusika katika magoli tisa katika mechi nane alizoanza katika Arsenal mashindano yote msimu huu

Arsenal wamefika robo fainali ya Kombe la FA baada ya kuwalaza Sutton United kupitia mabao ya Lucas Perez na Theo Walcott.

Katika mechi hiyo iliyochezewa Gander Green Lane, Wenger alifanya mabadiliko saba katika kikosi kilichochapwa 5-1 na Bayern Munich mechi ya mkondo wa kwanza hatua ya 16 bora katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wiki iliyopita.

Kikosi chake kilikuwa an nguvu za kutosha kuwazidi wapinzani hao ambao wamo nafasi 105 chini yao katika orodha ya ustadi wa klabu Uingereza.

Lucas Perez alifungia Arsenal bao la kwanza dakika ya 26 naye Theo Walcott akaongeza la pili dakika 10 baada ya kipindi cha pili kuanza.

Hilo lilikuwa goli lake la 100 kufungia Arsenal.

Ushindi huo ulimpunguzia shinikizo meneja Arsene Wenger.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Arsene Wenger aliteuliwa meneja wa Arsenal Septemba 1996

Arsenal sasa watakutana na Lincoln City katika robofainali.

Lincoln walifika robo fainali kwa kuwalaza Burnley Jumamosi.