Soulja Boy adai Chris Brown amejiondoa kutoka kwenye pigano

Soulja Boy

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwanamuziki Soulja Boy amedai kwamba Chris Brown amejiondoa kutoka kwenye pigano lao.

Wawili hao walikuwa wamezozana kwenye mitandao ya kijamii na baadaye wakaandaa pambano la ndondi kuamua nani mkali mjini Las Vegas.

Pambano hilo lingekuwa la raundi tatu. Hata hivyo, tarehe ya kufanyika kwa pigano hilo haikuwa imetangazwa.

Bingwa wa zamani wa ndondi duniani uzani wa heavyweight Mike Tyson alikuwa akimpa mafunzo Chris Brown naye Soulja Boy walikuwa akifunzwa na bingwa mwingine wa ndondi, Floyd Mayweather.

Lakini mwanarapa huyo ametangaza kupitia Twitter kwamba pigano hilo ambalo lilikuwa na dau ya $1m (£803,500) halitafanyika tena.

"Meneja wa Chris Brown alimpigia meneja wangu usiku wa kuamkia leo na kuniambia kwamba pigano halitafanyika tena na kwamba hatatia saini mkataba. Msiniulize zaidi."

Chanzo cha picha, AP

"Sitasema ... labda aliogopa, au labda hakukuwa na sababu yoyote. Nitasema tu kwamba hataki kupigana. Siwezi nikamlazimisha kutia saini mkataba."

Ugomvi kati ya wawili hao ulianza baada ya Soulja Boy kupenda na kutolea maoni picha ya Karrueche Tran, mpenzi wa zamani wa Chris Brown, kwenye Facebook.

Wawili hao walipakia kwenye Facebook video na picha wakitaniana na kutoleana vitisho.

Mwanarapa mwingine 50 Cent alibashiri Soulja Boy angeshinda na kusema angeweka dau ya $100,000 (£80,500).

Mike Tyson alitangaza kwenye mitandao ya kijamii kwamba alikuwa anarekodi wimbo wa kumshambulia Soulja Boy mwezi uliopita lakini kufikia sasa haujatolewa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Chris Brown, 27, na Soulja Boy, 26, wamekosolewa sana na mashabiki na wasanii wengine kwa kuweka hadharani ugomvi wao.

Wakili wa Chris Brown alitishia kumfikisha kortini Soulja Boy Januari.

Soulja Boy ametuhumiwa kutumia mechi hiyo kuongeza mauzo ya nyimbo zake na kujipatia umaarufu.

Kulikuwa pia na taarifa kwamba Soulja Boy alikuwa ameanza kufunzwa na bingwa mwingine wa zamani wa heavyweight Evander Holyfield, baada ya kukosana na Floyd Mayweather.