CAF: Hayatou kukabiliana na Ahmad kuwania urais

Amaju Pinnick
Maelezo ya picha,

Rais wa shirikisho la soka la Nigeria ,Amaju Pinnick

Shirikisho la soka la Nigeria (NFF) linamuunga mkono mpinzani wa rais aliyehudumu kwa muda mrefu Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou.

Bw Hayatou anawania kwa mara ya nane nafasi hiyo ya urais, licha ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa kiongozi wa shirikisho la soka la Madagascar Ahmad Ahmad.

Rais wa NFF, Amaju Pinnick , ameiambia BBC kwamba uchaguzi ''utakuwa wa muhimu sana kwa soka ya Afrika.''

Amesema Ahmad alikuwa ''mkakamavu'' kujitokeza kukabiliana na Bw Hayatou.

Pinnick amesema CAF inahitaji ''uongozi mpya'' kutoka kwa viongozi , baada ya mabadiliko yaliyofanyika katika bodi ya shirikisho la soka duniani Fifa.

Ametaja ''makabiliano ya baada ya uchaguzi kati ya Gianni Infantino, rais mpya wa Fifa, na Issa Hayatou kama ambayo hayawezi kutatuliwa.''

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Gianni Infantino

Infantino atakuwa mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini baadaye Jumanne kwa mkutano wa viongozi wa mashirikisho ya soka kutoka kote barani.

Baadaye anatarajiwa kutembelea Zimbabwe, kwa mwaliko kutoka kwa kiongozi wa shirikisho la soka la mataifa ya Afrika Kusini, Cosafa, linalomuunga mkono Ahmad.

Pinnick amekiri kwamba Hayatou bado angeibuka mshindi, lakini akasema iwapo atashinda atahitajika kuwa wazi kwa vishawishi vya aina yote.

''Lazima usikilize walio wengi na sio watu kadhaa, unastahili kufahamu kila kitu ni zaidi yako,'' Pinnick amesema.

''Nitafanya kazi naye, iwapo atashinda lakini maombi yangu tunahitaji mtu atakayeziba pengo na huyo mtu ni Ahmad.''