Ryan Giggs: Makocha wa nje Uingereza ni wengi mno

Ryan Giggs

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha,

Ryan Giggs alikuwa msaidizi wa Louis Van Gaal Manchester United

Ryan Giggs amesema anaamini kuna wakufunzi na mameneja wengi kupita kiasi katika Ligi Kuu ya Engalnd na kwamba Waingereza hawapewi nafasi.

Winga huyo wa zamani wa Manchester United na Wales amesema idadi kubwa ya wakufunzi hao kutoka nje inawanyima wenyeji nafasi ya kujiendeleza.

Giggs, 43, alikuwa kaimu meneja kwa mechi nne United baada ya David Moyes kufutwa mwaka 2014.

Baadaye alihudumu kama msaidizi wa Louis van Gaal.

"Sidhani kuna mameneja (Waingereza) wa kutosha ligini kwa sasa," alisema.

"Ni vyema kuona mkufunzi Mwingereza akipewa nafasi. Nafikiri ni muhimu. Kuna wakufunzi wengi wazuri kutoka nje Ligi ya Premia lakini pia kuna wakufunzi wengi na mameneja Waingereza huko nje."

Kwa sasa ni klabu saba pekee kati ya 20 zinazocheza EPL ambazo zina mameneja Waingereza.

Giggs, ambaye amesema hana haraka kurejelea kazi ya ukufunzi, amesema ufanisi wa Paul Clement katika Swansea City ni ishara wakufunzi Waingereza wanaweza kufanikiwa.

Ligini kwa sasa, klabu saba zilizo juu kwenye jedwali zimo chini ya wakufunzi kutoka nje. Wa juu zaidi ambao wamo chini ya Mwingereza ni West Brom ambao wamo chini ya Tony Pulis kutoka Wales.