Jamie Vardy awafaa Leicester Ligi ya Mabingwa Ulaya

Jamie Vardy

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Bao hilo la Jamie Vardy lilikuwa lake la kwanza tangu Desemba

Jamie Vardy afikisha kikomo ukame wake wa mabao uliodumu tangu Desemba kwa kufunga dhidi ya Sevilla na kuweka hai matumaini ya klabu hiyo Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Vardy alikuwa amecheza mechi tisa bila kufunga tangu alipofunga mabao matatu dhidi ya Manchester City tarehe 10 Desemba.

Lakini aliibuka tena na kufunga kutokana na krosi ya Danny Drinkwater zikiwa zimesalia dakika 17 ugenini Uhispania na kuwapa bao muhimu la ugenini ingawa walilazwa 2-1.

Sevilla walikuwa wameongoza 2-0 kutokana na mabao ya Pablo Sarabia na Joaquin Correa.

Kipa wa Leicester Kasper Schmeichel pia aliwafaa sana kwa kuokoa mkwaju wa penalti kutoka kwa Correa mabao yakiwa 0-0.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Kasper Schmeichel alikuwa amecheza dakika 385 bila kufungwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya

Mechi ya marudiano itachezwa uwanja wa King Power tarehe 14 Machi.