Wakala wa Wayne Rooney aenda China kujadili uhamisho

Wayne Rooney

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Rooney anashikilia rekodi ya ufungaji mabao United

Wakala wa Wayne Rooney Paul Stretford yupo nchini China kufanya mazungumzo kujaribu kuona iwapo atafanikiwa kuhamia klabu ya Ligi Kuu ya China.

Bado hakuna hakikisho lolote la mafanikio na duru zinasema huenda ikawa vigumu kwake kufanikiwa kuhamia huko kabla ya muda wa wachezaji kuhama China kumalizika tarehe 28 Februari.

Lakini hali kwamba Stretford amesafiri China ni ishara wazi kwamba meneja wa Manchester United Jose Mourinho anaweza kumwacha Rooney, 31, ahame.

Na iwapo hatafanikiwa kuhama mwezi huu, basi bila shaka atahama majira ya joto.

Rooney ameshuka hadhi United chini ya Mourinho na amekuwa hapati nafasi ya kuanza kwenye kikosi.

Nahodha huyo wa England alifahamishwa mapema kwamba anatafutwa na klabu za China, ingawa haijabainika ni klabu gani zinamtaka.

Beijing Guoan, klabu ambayo inadhaniwa kupendwa sana na Rais wa China Xi Jinping, ni moja ya zinazopigiwa upatu kutaka kumnunua Rooney lakini kuna duru zimeambia BBC kwamba kwa sasa hawataki kumnunua.

Kutokana na masharti yaliyowekewa klabu za China kuhusu wachezaji wa kutoka nje, klabu za Jiangsu Suning na Tianjin Quanjian ndizo pekee zinazoonekana kuwa na nafasi ya kutaka kumnunua.

Wawakilishi wa Rooney tayari wamefanya mazungumzo na Tianjin Quanjian na kocha wao Fabio Cannavaro alisema mazungumzo yao hayakuzaa matunda.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Oscar wa Chelsea alihamia Shanghai SIPG kwa £60m Desemba na alifunga mechi yake ya kwanza Chelsea